SOMO LA KWANZA
1 Samueli 24:3—21
Somo kutoka Kitabu cha kwanza cha Samueli.
Siku zile: Sauli aliwachukua watu elfu tatu katika Israeli yote, akaondoka nao kumtafuta Daudi na wafuasi wake upande wa mashariki wa mwamba wa Mbuzimawe. Na alipofika mahali penye mazizi ya kondoo kando ya njia, palikuwa na pango. Sauli akayasikiliza akaingia humo ili kuifunika miguu. Daudi na watu wake walikuwa wamekaa humo pangoni kwa ndani sana. Watumishi wa Daudi kwa wakamwambia, "Tazama, hii ndiyo siku ile Bwana alipokuambia: Ndimi ninayemtia adui yako mikononi mwako; na utende upendavyo!" Basi Daudi akainuka, akaukata upindo wa bushuti la Sauli kwa siri. Naye akawaambia watu wake, "Hasha! Nisimtende bwana wangu, masiya wa Bwana, neno hili, kunyoosha mkono wangu juu yake; kwa maana yeye ni mpakwa wa Bwana." Akiisha kusema hayo, Daudi aliwazuia watu wake, wala hakuwaruhusu kumshambulia Sauli. Naye Sauli akatoka pangoni akaenda zake. Daudi naye pia akatoka nje ya pango, akamwita Sauli kwa sauti kuu, "Ee bwana wangu mfalme," Sauli alipogeuka nyuma, tazama Daudi aliinama chini akasujudu. Ndipo alipomwambia Sauli, "Mbona unawasikiliza watu wasemao ya kuwa Daudi anatafuta kukudhuru? Wewe mwenyewe leo umejionea kuwa Bwana amekutia mikononi mwangu katika pango hili. Nilifikiria kukuua, lakini nilikuhurumia. Nikaamua kukuacha, nikisema, 'Sitaki kuunyosha mkono wangu juu ya bwana wangu, kwa maana yeye ni mpakwa wa Bwana, na baba kwangu.' Tazama upindo huu wa bushuti yako mikononi mwangu, maana ikiwa nimeukata upindo wa vazi lako, nisikuue, ujue na kuona ya kuwa hakuna uovu ndani yangu ili kunidhuru. Bwana na atuamue mimi na wewe, Bwana mwenyewe akulipize kisasi kwa ajili yangu, lakini mkono wangu hautakugusa. Kama isemavyo mithali ya kale, 'katika waovu, hutoka uovu,' lakini mkono wangu hautakugusa. Basi, mfalme wa Israeli ametoka ili kumfuata nani? Unawinda nani? Unamwinda mbwa, mfu au kiroboto? Bwana na atuamue, akatuhukumu, mimi na wewe, akaone, akanitetee neno langu, na akaniokoe na mkono wako." Daudi alipokwisha kusema hivyo, Sauli akajibu, "Hii ndiyo sauti yako, Daudi mwanangu?" Naye akalia kwa sauti. Sauli akamwambia Daudi, "Wewe u mtu mwenye haki kuliko mimi, maana umenitendea mema, nami nimekutendea mabaya. Leo umenionyesha uwingi wa wema wako, kwa maana Bwana aliniacha mikononi mwako lakini wewe hukuniua. Kama mtu amekutana na adui yake, atamwacha aende zake tu salama? Basi Bwana na akutuze mema kwa hayo uliyonitendea leo. Na sasa, tazama, ninajua ya kuwa hakika utakuwa mfalme, na ufalme wa Israeli utakaa imara mikononi mwako."
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 57:2, 3—4, 6 na 11 (K. 2a)
K. Unihurumie, ee Mungu, unihurumie.
Unihurumie, ee Mungu, unihurumie,
kwa maana nafsi yangu imekukimbilia wewe.
Ninakimbilia kivulini mwa mbawa zako,
mpaka msiba huu utakapopita. K.
Ninakulilia Mungu Uliye Juu,
Mungu anitendeaye mema.
Mungu apeleke wokovu toka mbinguni,
awatie aibu wenye kunidhulumu.
Mungu alete upendo uliojaa huruma na uaminifu. K.
Utukuzwe ee Mungu, juu ya mbingu;
utukufu wako ung'are juu ya dunia!
Maana wema wako waenea hadi mbinguni,
na ukweli wako mpaka mawinguni. K.
SHANGILIO LA INJILI
2 Wakorintho 5:19
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mungu ameupatanisha ulimwengu na nafsi yake katika Kristo, akaliweka neno la upatanisho ndani yetu.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 3:13—19
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Wakati ule: Yesu alipanda mlimani, akawaita kwake wale aliowapenda; nao wakamjia. Aliwateua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume, wawe naye kusudi awatume kuhubiri, na awape uwezo wa kuponya magonjwa na kuwatoa pepo wabaya. Basi, hao kumi na wawili walioteuliwa ni hawa: Simoni, ambaye Yesu alimpa jina la Petro; Yakobo, mwana wa Zebedayo, na Yohane nduguye Yakobo, ambao aliwapa jina Boanerge, maana yake, wana wa ngurumo; Andrea, Filipo, Bartolomayo, Mathayo, Tomaso, Yakobo, mwana wa Alfayo; Thadei, Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, ambaye alimsaliti.
Injili ya Bwana