SOMO LA KWANZA
1 Samueli 18:6—9, 19:1—7
Somo katika kitabu cha kwanza cha Samueli
Siku zile: Wakati Daudi alipokuwa anarejea kutoka kumwua yule Mfilisti, wanawake walitoka katika miji yote ya Israeli kwenda kumlaki mfalme Sauli huku wakiimba na kucheza; wakiwa na matari, vigelegele na vinanda. Hao wanawake walicheza na kuitikiana, wakisema, "Sauli amewaua elfu zake, na Daudi makumi elfu zake." Basi Sauli alifadhaika sana na kuchukizwa na maneno hayo; akasema, "Wamempa Daudi elfu kumi, nami wamenipa elfu tu! Anahitaji kupata nini tena isipokuwa ufalme tu!" Tangu siku ile,Sauli akamwonea wivu Daudi. Sauli akasema na mwanaye Yonathani, watumishi wake wote juu ya kusudio lake la kumwua Daudi. Lakini Yonathani, mwana wa Sauli, alimpenda sana Daudi, naye akampasha habari hiyo, akisema, "Sauli baba yangu, anatafuta kukuua; basi nakusihi uwe macho asubuhi, ukajifiche mahali pa siri. Nami nitatoka na kusimama kando ya babangu huko shambani ulipo wewe, na nitazungumza naye habari zako. Nikiona jambo lolote nitakuambia." Yonathani akamsifia Daudi kwa Sauli babaye, akisema, "Mfalme na asikose juu ya mtumishi wake Daudi, kwa kuwa yeye hakukosa juu yako, bali matendo yake kwako yamekuwa mema sana. Aliyahatarisha maisha yake, akamwua yule Mfilisti, naye Bwana akawaletea Waisraeli wote ushindi mkuu. Nawe mwenyewe ulipoona hayo ukafurahi, basi kwa nini kukosa juu ya damu isiyo na hatia, umwue Daudi bure?" Sauli akayasikiliza maneno ya Yonathani kwa makini, akaapa, "Aishivyo Bwana, hatakufa!" Ndipo Yonathani akamwita Daudi, akamjulisha maneno yale yote. Yonathani Akamleta Daudi kwa Sauli, naye akamtumikia kama kwanza.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 56:2—3, 9—10ab, 10c—11, 12—13
K. Ninamtumainia Mungu sitaogopa.
Unihurumie, ee Mungu, kwani wananitendea kwa ukali;
mchana kutwa wanazidi kunipiga vita.
Mchana kutwa adui zangu wananisaka:
maana ni wengi wanaonipiga vita, ewe Uliye Juu. K.
Umezihesabu hatua za kutangatanga kwangu;
umepokea machozi yangu, umeyakusanya;
Je, si yameandikwa katika kitabu chako?
Hapo maadui wangu watarudi nyuma
siku ninapoomba msaada wako. K.
Najua hakika Mungu yupo upande wangu.
Ninasifu neno la Mungu, ninasifu neno lake Bwana. K.
Namtumainia Mungu, wala siogopi kitu.
Mwanadamu ataweza kunitenda nini?
Ee Mungu, nimebanwa na nadhiri zangu kwako.
Nitakutolea dhabihu za sifa. K.
SHANGILIO LA INJILI
K. Aleluya. A. Aleluya
K. Mwokozi wetu Kristo Yesu ameyashinda mauti na ametangaza uzima wa milele kwa Injili.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 3:7—12
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Wakati ule:Yesu aliondoka akaenda kando ya ziwa pamoja na wafuasi wake. Umati mkubwa ulimfuata kutoka Galilaya na kutoka Yudea. Pia wengine kutoka Yerusalemu na wengine kutoka Idumea, na ng'ambo ya Yordani, na kutoka sehemu ya Tiro na Sidoni, umati mkubwa ukamjia waliposikia aliyokuwa akifanya. Akawaambia wafuasi wake wamwekee chombo tayari kwa sababu ya umati wa watu, wasije wakamsonga. Maana aliponya wengi, hata wote walioshikwa na mateso yoyote walisogea mbele wapate kumgusa. Na pepo wachafu walipomwona walimwangukia, wakagumia wakisema,'Wewe ni Mwana wa Mungu." Akawakataza sana wasimtambulishe.
Injili ya Bwana.