SOMO LA KWANZA
1 Samueli 17:32—33, 37, 4—51
Somo katika kitabu cha kwanza cha Samueli
Siku zile: Daudi alimwambia Sauli, “Asivunjike moyo mtu yeyote kwa ajili ya huyu; maana mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana na Mfilisti huyu.” Lakini Sauli akamwambia Daudi, “Huwezi wewe kumwendea huyu Mfilisti na kupigana naye, maana u kijana bado, na huyu mtu ni wa vita tangu ujana wake.” Daudi akaendelea kusema, “Bwana aliyeniokoa katika makucha ya simba na dubu, ataniokoa pia na mkono wa huyu Mfilisti.” Sauli akamjibu Daudi, “Nenda, na Bwana atakuwa pamoja nawe.” Daudi akaichukua fimbo yake mkononi, na alajichagulia mawe laini matano katika kijito cha maji, akayatia katika mfuko wake wa kichungaji, akalitwaa kombeo lake mkononi, akamwendea Mfilisti. Naye Mfilisti akitanguliwa na mtumishi wake akamsogelea Daudi zaidi na zaidi. Mfilisti yule akamtazama Daudi kwa makini, akamdharau kwa maana alikuwa ni kijana tu, mwekundu na mwenye sura nzuri. Mfilisti akamwambia, “Je, mimi ni mbwa hata umenijia na fimbo?” Kisha Mfilisti akamwapiza Daudi kwa miungu yake, na akamwambia Daudi, “Njoo kwangu, huku nami nitawapa nyama yako ndege wa angani na wanyama wa porini.” Naye Daudi akamjibu Mfilisti, “Wewe unanijia mimi na upanga, mkuki na sagai, lakini mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Leo Bwana atakutoa mikononi mwangu, nami nitakupiga, nitakuua na kukukata kichwa. Leo hii nitawapa ndege wa angani na wanyama wa porini mzoga wa maiti yako na mizoga ya maiti ya Wafilisti, ili dunia nzima wajue ya kuwa kuna Mungu katika Israeli. Nao umati wote huo watajua kuwa Bwana haokoi kwa upanga au kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana naye atawatia ninyi mikononi mwetu.” Mfilisti akatoka mbio jeshini ili kukutana na Mfilisti. Daudi akautia mkono wake katika mkoba wake, akatwaa humo jiwe moja, na akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti kwenye paji la uso wa jiwe hilo likamwingia pajini mwa uso wake, akaanguka kifudifudi. Hivyo Daudi akamshinda Mfilisti kwa kombeo na jiwe; akampiga Mfilisti na kumwua bila kuchukua upanga mkononi mwake. Ndipo Daudi akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti, akauchomoa upanga wake akaufuta alani mwake, akamwua na kumkata kichwa. Wafilisti walipoona shujaa wao amekufa wakakimbia.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 144:1, 2, 9—10 (K. 1a)
K. Atukuzwe Bwana, mwamba wangu.
Atukuzwe Bwana, mwamba wangu,
Aipaye mikono yangu mazoezi kwa ajili ya vita,
Na vidole vyangu kwa ajili ya kupigana. K.
Mhisani wangu na boma langu;
Ngome yangu na mwokozi wangu;
Ngao yangu ninayemkimbilia,
Anayetiisha watu chini yangu. K.
Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya;
Nitakupigia kinubi cha nyuzi kumi.
Ndiwe uwapao wafalme ushindi,
Ulimwopoa Daudi, mtumishi wako, na upanga hatari. K.
SHANGILIO LA INJILI
Mathayo 4:23
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Yesu alitangaza Injili ya ufalme na kuponya kila ugonjwa na maradhi ya watu.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 3:1—6
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Wakati ule: Yesu aliingia katika sinagogi. Humo alikuwamo mtu mwenye mkono uliopooza. Wakaangalia waone kama atamponya siku ya sabato, wapate kumshitaki. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Simama mbele yetu.” Kisha akawauliza, “Je, ni halali kutenda mema siku ya Sabato au kutenda mabaya? Kuyaokoa maisha au kuyaangamiza? Lakini wakanyamaza. Akiisha kuwakazia macho pande zote kwa hasira, huku akihuzunishwa sana kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao, alimwambia yule mtu, “Unyooshe mkono wako.” Naye akaunyosha, mkono wake ukawa mzima tena. Mafarisayo wakatoka, wakaanza mara kushauriana na Maherodi dhidi yake, jinsi ya kumwangamiza.
Injili ya Bwana.