SOMO LA KWANZA
1 Samueli 15:16—23
Somo katika kitabu cha kwanza cha Samueli
Siku zile: Samueli alimwambia Sauli, “Acha! Ngoja nami nikuambie neno alilonifunulia Bwana usiku huu.” Naye akajibu, “Sema!” Samueli akasema tena, “Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je, hukufanywa kuwa kichwa cha makabila ya Israeli? Bwana amekutia mafuta uwe mfalme wa Israeli. Na akakutuma kushambulia akikuambia: Ondoka ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hata waangamie. Mbona basi, hukumtii Bwana? Ukazirukia nyara, na kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana?” Sauli akamjibu Samueli, “Nimemtii Bwana! Nimewashambulia wale alioniagiza, nikamleta Agagi, mfalme wa Amaleki, nikawaangamiza kwa laana. Lakini nyara zile, watu waliwachagua wanyama bora zaidi kutoka vitu vilivyopaswa laana, ili kuwatoa sadaka kwa Bwana Mungu wako huko Giligali.” Lakini Samueli akasema, “Je, Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu sawasawa na utii kwa amri yake? Tazama, kutii ni bora kuliko sadaka, na kusikia kuliko mafuta ya kondoo dume. Kwa maana kuasi ni kama dhambi ya ushirikina, na ukaidi ni kama kosa la kuabudu sanamu. Kwa vile umelikataa neno la Bwana yeye naye amekukataa kama mfalme.”
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
50:8—9, 16bc—17, 21 na 23 (K. 23bc)
K. Yeye ambaye mwenendo wake hauna hatia, nitamwonyesha wokovu wa Mungu.
Sikukaripii kwa ajili ya matoleo yako,
Sadaka zako za kuteketeza zipo mbele yangu daima.
Sitapokea fahali kutoka mashambani mwako,
Wala beberu kutoka kwenye mazizi yako. K.
Unawezaje kuzikariri sheria zangu,
Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
Wewe unayeyadharau maonyo,
Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako! K.
Unafanya haya, nami ninyamaze?
Unadhani ya kuwa mimi ni kama wewe?
Ninakushitaki: ninayaweka mashtaka hayo mbele yako.
Sadaka ya sifa, ndiyo inayonipa heshima;
Naye ambaye mwenendo wake hauna hatia,
Nitamwonyesha wokovu wa Mungu. K.
SHANGILIO LA INJILI
WAEBRANIA 4:12
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Neno la Mungu ni hai, tena lina nguvu, laweza kupambanua nia na maono ya moyo.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 2:18—22
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Wakati ule, wafuasi wa Yohane na wa Mafarisayo walikuwa katika kufunga. Wakaja watu wakamwambia [Yesu], “Kwa nini wafuasi wa Yohane na wafuasi wa Mafarisayo wanafunga, lakini wafuasi wako hawafungi?” Yesu akawaambia, “Je, wana harusi waweza kufunga wakati bwana harusi yupo pamoja nao? Muda wote walipo na bwana harusi hawawezi kufunga. Lakini siku zitakuja atakapoondolewa bwana harusi kwao, ndipo watakapofunga siku ile. Hakuna ashonaye kiraka cha nguo mpya katika nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, kiraka cha nguo mpya kitajitoa katika nguo iliyochakaa, na mpasuko mbaya utatokea. Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, divai mpya itavipasua viriba, hivyo viriba na divai vitapotea. Divai mpya hutiwa katika viriba vipya.”
Injili ya Bwana.