SOMO LA KWANZA
1 Samueli 3:1—10, 19
Somo katika kitabu cha kwanza cha Samueli
Siku zile: Samueli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, pale lilipokuwapo sanduku la Bwana. Bwana akaita: Samueli, Samueli, naye akaitikia, "Mimi hapa!" Naye akamwendea Eli kwa haraka akasema, "Mimi hapa, kwa kuwa uliniita." Eli akasema, "Sikukuita, nenda ukalale." Akaenda kulala. Bwana akaita tena: Samueli, Samueli! Naye akamwendea tena Eli, na kusema, "Mimi hapa, kwa maana uliniita!" Naye akajibu, akasema, "Sikukuita mwanangu, nenda ukalale." Wakati ule Samueli alikuwa bado hajamfahamu Bwana, na neno la Bwana lilikuwa bado kufunuliwa. Bwana akamwita tena Samueli mara ya tatu. Hapo aliamka na kumwendea Eli akasema, "Mimi hapa, kwa maana uliniita." Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita kijana. Akamwambia Samueli, "Nenda ukalale na utakapoitwa, utasema, 'Nena Bwana kwa kuwa mtumishi wako anasikia.'" Basi akaenda kulala mahali pake. Bwana akaja, akasimama, na kuita kama awali: Samueli Samueli! Ndipo Samueli akaitikia, "Nena Bwana kwa kuwa mtumishi wako anasikia." Samueli akakua, na Bwana alikuwa pamoja naye, wala hakuacha neno lolote lianguke chini.
Neno la Bwana .
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 40:2 na 4ab, 7—8a, 8b—9, 10 (K. 8a, 9a)
K. Tazama, nimekuja kuyatimiza mapenzi yako, ee Bwana.
Nalimngojea Bwana kwa subira;
akanielekea na kukisikia kilio changu,
akaweka wimbo mpya kinywani mwangu,
sifa za Mungu wetu. K.
Hukupenda sadaka wala matoleo;
ila masikio wazi kwa kutii;
hukutaka dhabihu za kuteketeza wala sadaka za dhambi;
hapo nilisema, "Mimi hapa, nimekuja." K.
Katika gombo la chuo nimeandikiwa amri zako.
"Napenda kutimiza mapenzi yako,
ee Mungu wangu, sheria yako imo moyoni mwangu!" K.
Nitatangaza habari ya haki yako
katika mkutano mkubwa;
wala sikuzuia midomo yangu,
ee Bwana, wewe wajua. K.
SOMO LA PILI
1 Wakorintho 6:13c—15a, 17—20
Somo katika barua ya kwanza ya Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho
Ndugu zangu: Mwili si kwa ajili ya anasa, bali kwa ajili ya Bwana, na Bwana ni kwa ajili ya mwili. Na Mungu aliyemfufua Bwana, naye atatufufua sisi pia kwa uwezo wake. Je hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Lakini yeye anayeambatana na Bwana ni roho moja naye. Ikimbieni zinaa. Makosa yote ayatendayo mwanadamu yapo nje ya mwili, ila mwenye kuzini huukosea mwili wake wenyewe. Au hamjui ya kuwa miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu? Mwili mmepewa na Mungu! Kwa hiyo si mali yenu. Maana mmenunuliwa kwa bei kubwa. Basi mtukuzeni Mungu katika miili yenu.
Neno la Bwana.
SHANGILIO LA INJILI
Yohane 1:41, 17b
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Tumemwona Masiya, ndiye Kristo; neema na kweli zimepatikana kupitia yeye.
W. Aleluya.
INJILI
Yohane 1:35—42
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Yohane
Wakati ule: Yohane alisimama tena huko pamoja na wawili wa wanafunzi wake; akamwona Yesu akipita njiani, akasema, "Tazameni, Mwanakondoo wa Mungu!" Wale wafuasi wake wawili waliposikia hayo walimfuata Yesu. Yesu akageuka, akawaona wanamfuata, akawauliza, "Mnatafuta nini?" Nao wakajibu, "Rabbi," inayotafsiriwa, Mwalimu, "Unakaa wapi?" Akawaambia, "Njoni, mtaona." Wakafuatana naye, wakaona, wakashinda kwake siku ile. Ilikuwa saa kumi. Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliomsikia Yohane na kumfuata Yesu. Huyo alikutana kwanza na Simoni, nduguye, akamwambia, "Tumemwona Masiya," (inayotafsiriwa, Kristo). Akampeleka kwa Yesu. Yesu akamtazama, akasema, "Wewe u Simoni, mwana wa Yohane; utaitwa Kefa," inayotafsiriwa, Petro.
Injili ya Bwana.