SOMO LA KWANZA
1 Samueli 9:1—4, 17—19, 26a; 10:1a
Somo katika kitabu cha kwanza cha Samueli.
Kulikuwa na mtu mmoja wa Benjamini, jina lake Kishi, mwana wa Abeli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, wa ukoo wa Benjamini. Naye alikuwa na mwana, aliyeitwa jina lake Sauli, mtu mwenye sura nzuri, wala katika wana wa Israeli hakuwako mtu aliye mzuri kuliko yeye; tena toka mabega yake kwenda juu alikuwa mrefu kuliko wote. Ikawa punda wa Kishi, baba yake Sauli, walikuwa wamepotea. Kisha akamwambia, Sauli mwanawe, "Twaa mtumishi mmoja pamoja nawe, uondoke, ukawatafute punda hao." Nao wakaondoka, wakavuka nchi ya vilima ya Efraimu, wakapita nchi ya Shalisha, lakini hawakuwapata. Wakapita nchi ya Shaalimu hawakuwako, na wakapita nchi ya Benjamini lakini hawakuwapata. Samueli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia: Huyu ndiye niliyekuambia habari zake, ndiye atakayewamiliki watu wangu. Sauli akamkaribia Samueli, katikati ya malango akasema, "Tafadhali niambie anapoishi mwonaji." Samueli akajibu, "Mimi ndimi mwonaji. Tangulia mbele yangu na ukwee mpaka mahali pa kuabudia! Kwa maana leo utakula pamoja nami. Kesho asubuhi nitakuruhusu uende zako, na kukueleza yote yaliyomo moyoni mwako. Mapema kulipopambazuka alfajiri, Samueli akatwaa kichupa cha mafuta, akayamimina kichwani pa Sauli.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 21:2—3, 4—5, 6—7 (K. 2a)
K. Ee Bwana, mfalme anafurahi katika nguvu yako.
Ee Bwana, mfalme anafurahi katika nguvu yako;
anaushangilia sana ushindi wako!
Umemtimizia matashi ya moyo wake;
wala hukumkatalia sala ya midomo yake. K.
Maana umemjalia baraka za heri;
umemvika taji la dhahabu safi kichwani mwake.
Alikuomba uhai na ukamjalia;
ukampa wingi wa siku milele na milele. K.
Kwa msaada wako, utukufu wake umeongezeka;
umeweka juu yake ukuu na utukufu.
Umemjalia baraka hata milele,
umemfurahisha kwa furaha ya uwepo wako. K.
SHANGILIO LA INJILI
Luka 4:18
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Bwana amenituma niwahubirie maskini habari njema, kuwatangazia wafungwa kufunguliwa.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 2:13—17
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Wakati ule: Yesu alitoka tena kwa kupitia kandoni mwa ziwa. Kundi lote la watu likamwendea, naye akawafundisha. Alipokuwa akipita njiani, alimwona Lawi, mwana wa Alfayo, ameketi forodhani. Akamwambia, "Nifuate." Naye akasimama, akamfuata. Baadaye Yesu alipokuwa mezani nyumbani mwake, watoza ushuru wengi na wakosefu waliketi pamoja na Yesu na wafuasi wake; kwa maana wengi wao walimfuata. Baadhi ya Waandishi waliokuwa Mafarisayo walipomwona anakula pamoja na watoza ushuru na wakosefu, waliwaambia wafuasi wake, "Kwa nini mnakula na kunywa pamoja naa watoza ushuru na wadhambi?" Yesu alisikia hayo, akawaambia, "Wenye afya hawahitaji tabibu, bali wagonjwa. Sikuja kuwaita waadilifu, bali wadhambi."
Injili ya Bwana.