SOMO LA KWANZA
1 Samueli 8:4—7, 10—22a
Somo katika kitabu cha kwanza cha Samueli
Siku zile: Wazee wote wa Israeli wakakutana na wakamwendea Samueli huko Rama. Nao wakamwambia, "Wewe sasa umekuwa mzee na wanao hawafuati mfano wako, basi utupatie mfalme, atutawale kama mataifa mengine yote." Lakini maneno hayo: "Utupe mfalme atuamue," yalimchukiza Samueli, hata akamwomba Bwana, naye Bwana akamwambia Samueli: Sikiliza kila neno utakaloambiwa na watu hao, maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi ili nisiwe mfalme juu yao. Hivyo, Samueli akawaambia maneno yote ya Bwana watu wale waliokuwa wakimwomba mfalme. Akawaambia, "Mfalme atakayewamiliki ninyi atakuwa na desturi hii: atatwaa wana wenu na kuwaweka kwa magari yake, atawaweka kuwa maakida juu ya watu elfu, na juu ya maaskari mia, atawatumikisha kulima mashamba yake, na kuvuna mavuno yake, na kufanya silaha zake za vita na vyombo vya magari yake. Na atawatwaa binti zenu kuwa watengeneza manukato, na wapishi na waoka mikate. Atatwaa makonde yenu, na mashamba yenu ya mizabibu, na ya mizeituni yaliyo bora zaidi na kuwapa watumishi wake. Atawatoza ushuru kwa mazao yenu, na mizabibu yenu na kuwapa maakida na watumishi wake. Atawatwaa watumishi wenu na wajakazi wenu, naye atawatumikisha kwa kazi zake. Atawatoza fungu la kumi kwa mifugo yenu na ninyi wenyewe mtakuwa watumwa wake. Litakapotokea neno hili mtalalamika kwa sababu ya mfalme mliyejichagulia, lakini Bwana hatawajibu." Watu, lakini, walikataa kumsikiliza Samueli; wakasema, "Sivyo hivyo! Sisi tunataka mfalme juu yetu; ili nasi tufanane pia na mataifa yote, maana mfalme wetu atatuamua, atatoka mbele yetu na kupiga vita vyetu." Samueli akayasikia maneno yote ya watu, akayanena masikioni mwa Bwana. Ndipo Bwana akamwambia Samueli: Uisikilize sauti yao na uwasimikie Mfalme."
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 89:16—17, 18—19 (K. 2a)
K. Fadhili zako nitaziimba milele, ee Bwana.
Heri taifa linalozijua sifa zako,
waendao, ee Bwana, katika mwanga wako.
Wanafurahishwa na jina lako mchana kutwa;
nao kwa haki yako wanakutukuza kwa kushangilia. K.
Kwa maana wewe ni utukufu wa nguvu yao;
na kwa fadhili yako unainua moyo wetu.
Maana Bwana ni ngao yetu,
na Mtakatifu wa Israeli, mfalme wetu! K.
SHANGILIO LA INJILI
LUKA 7:16
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Nabii mkubwa ametokea kwetu, na Mungu amewaangalia watu wake.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 2:1—12
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Baada ya siku kadhaa, Yesu aliporudi tena Kapernaumu, habari ikavuma ya kwamba alikuwamo nyumbani. Mara watu wengi wakakusanyika, isibaki nafasi hata mlangoni. Alikuwa akiwahubiria neno. Wakamletea mtu mwenye kupooza akichukuliwa na watu wanne. Nao wakishindwa kumpeleka kwake kwa sababu ya msongamano wa watu, waliezua dari juu ya mahali alipokuwa amesimama, wakamteremsha mgonjwa pamoja na mkeka aliolalia. Yesu alipoona imani yao, alimwambia mwenye kupooza, "Mwanangu, umeondolewa dhambi zako." Lakini baadhi ya Waandishi walikuwa wamekaa hapo wakijiuliza mioyoni mwao, "Kwa nini mtu huyu anakufuru hivi? Nani aweza kuondolea dhambi isipokuwa Mungu peke yake?" Mara Yesu akang'amua mawazo yao rohoni mwake, basi akasema, "Kwa nini mnafikiri hivyo mioyoni mwenu? Je, ni kipi chepesi zaidi, kumwambia mwenye kupooza, 'umeondolewa dhambi zako' au kusema, 'Simama, jitwike mkeka wako, uende?' Basi, mpate kujua ya kuwa Mwana wa Mtu anao uwezo wa kuondolea dhambi duniani" alimwambia mwenye kupooza, "Nakuambia, simama, jitwike mkeka wako, nenda nyumbani mwako." Mara akasimama, akajitwika mkeka wake, akatoka mbele yao. Wote wakashangaa, wakamtukuza Mungu, wakisema, "Kamwe hatujapata kuona hivi."
Injili ya Bwana.