SOMO LA KWANZA
1 Samueli 4:11
Somo katika kitabu cha kwanza cha Samueli
Ikawa siku zile Israeli alitoka kwenda kwenye vita dhidi ya Wafilisti; nao wakapiga kambi karibu na Ebenezeri, nao Wafilisti walipiga kambi yao huko Afeka. Wafilisti wakajipanga juu ya Waisraeli na kupigana nao, pakawa na mapigano makali sana; mwishowe Waisraeli wakashindwa na Wafilisti, wakauawa watu wa jeshi lao wapatao elfu nne katika uwanja wa vita. Pale jeshi liliporudi kambini, wazee wa Israeli wakasema, "Mbona Bwana ametupiga leo mbele ya Wafilisti? Haya twende tukalilete sanduku la agano la Bwana kutoka Shilo hata liwe kati yetu na kutuokoa katika mikono ya adui zetu." Ndipo wakawatuma watu Shilo kulileta sanduku la agano la Bwana wa majeshi akaaye juu ya Makerubi. Wana wawili wa Eli, Hofini na Finehasi walikuwa huko wakifuatana na sanduku la agano la Bwana. Na sanduku la agano la Bwana lilipoingia kambini, Waisraeli wote walipiga kelele kwa sauti kuu, hata nchi ikatetemeka. Nao Wafilisti waliposikia mshindo wa kelele zile, wakasema, "Mshindo huu wa kelele kambini mwa Waisraeli maana yake nini?" Wakatambua ya kuwa sanduku la agano la Bwana limefika kambini. Wafilisti wakaogopa sana wakasema, "Ole wetu! Maana miungu wamekuja kambini. Halijawahi kutokea jambo kama hilo hapo awali. Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa mikononi mwa miungu hawa walio na uwezo? Hawa ndio miungu waliowapiga Wamisri kwa mapigo na misiba ya kila namna. Jipeni moyo na kuwa hodari kama wanaume, enyi Wafilisti, msije mkawa watumwa wa Waebrania kama wao walivyo watumwa wenu; mkapigane nao kiume!" Wafilisti wakapigana nao, na Waisraeli wakashindwa wakakimbia kila mtu hemani mwake; kulikuwa msiba mkuu maana askari thelathini elfu wa Israeli waendao kwa miguu waliuawa siku ile. Na hilo sanduku la Mungu nalo likatekwa, na Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwa kati ya wale waliouawa.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 44:10—11, 14—15, 24—25 (K. 27b)
W. Utuokoe ee Bwana, kwa upendo wako uliojaa rehema!
Bwana, umetuacha na kutudhalilisha;
wala hutoki tena na majeshi yetu.
Umeturudisha nyuma ya adui zetu;
wanaotuchukia wanateka mali zetu wanavyopenda. K.
Umetufanya kuwa kichekesho kwa jirani zetu,
dharau na bezo kwa watuzungakao.
Umetufanya kuwa uvumi kwa mataifa;
watu wanatikisa vichwa juu yetu. K.
Amka! Ee Bwana, mbona unalala?
Inuka! Usitutupe milele!
Mbona unauficha uso wako;
na kuusahau umaskini wetu na kukandamizwa kwetu? K.
SHANGILIO LA INJILI
Mathayo 4:23
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Yesu alitangaza Injili ya ufalme na kuponya kila ugonjwa katika watu.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 1:40—45
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Wakati ule: Mtu mwenye ukoma alimjia Yesu, akampigia magoti na kusema, "Ukitaka, waweza kunitakasa." Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa na kumwambia, "Nataka, takasika." Mara hapo ukoma ukamtoka, akatakasika. Alipokwisha kumwonya akamwacha aende zake. Na akamwambia, "Angalia, usimweleze mtu chochote, isipokuwa nenda ukajionyeshe kwa kuhani utoe zaka iliyoamriwa na Musa kwa kupona ukoma wako; kusudi iwe ushuhuda kwao." Huyo lakini alitoka, akaanza kutangaza wazi na kulieneza tukio hilo, kiasi kwamba Yesu hakuweza tena kuingia mjini. Basi, akakaa nje mahali pa ukiwa. Hata hivyo watu walimwendea kutoka pande zote.
Injili ya Bwana.