SOMO LA KWANZA
1 Samueli 1:9—20
Somo katika kitabu cha kwanza cha Samueli
Siku zile: Baada ya chakula kule Shilo, Hana aliinuka na kwenda kuomba mbele ya Bwana; na wakati huo, Eli kuhani alikuwa ameketi mlangoni pa hekalu la Bwana. Kwa uchungu wa moyoni Hana aliomba na kulia mbele ya Bwana, na akaweka nadhiri hii: "Ee Bwana wa majeshi, kama wewe utaangalia mateso ya mjakazi wako na kunikumbuka, bila kumsahau mjakazi wako na kumpa mtoto wa kiume, basi nami nitamtolea Bwana siku zote za maisha yake; hatakunywa divai wala kileo, na wala wembe hautamgusa kichwa kabisa." Kwa vile alivyobaki muda mrefu mbele ya Bwana huku akiomba, Eli aliutazama mdomo wake, kwa maana Hana alisali kimya kimya; ingawa midomo yake ilionekana kunena, sauti yake haikusikika. Eli akadhani kuwa amelewa, ndipo alipomwambia, "Je, utakuwa mlevi hata lini? Acha ulevi wako wa divai!" Si hivyo bwana wangu," Hana akamjibu, "mimi ni mwanamke mwenye huzuni tele moyoni. Sikunywa divai wala kileo; ila nimeimimina roho yangu mbele ya Bwana. Usimdhanie mjakazi wako kuwa mwanamke asiyefaa kitu, kwa kuwa katika wingi wa kuugua na kusikitika kwangu, ndivyo nilivyonena mbele ya Bwana hata sasa." Eli akamwambia, "Enenda zako kwa amani, Mungu wa Israeli akujalie haja yako ulivyomwomba." Naye akasema, "Mjakazi wako na aone kibali machoni pako." Basi huyo mwanamke akaenda zake, akala chakula pamoja na mumewe, na uso wake haukuwa umekunjamana tena. Mapema asubuhi kesho yake, wakaabudu mbele ya Bwana, na wakarudi nyumbani kwao kule Rama. Elkana akamjua Hana mkewe naye Bwana akamkumbuka. Na wakati ulipowadia Hana akashika mimba, akamzaa mtoto wa kiume, akamwita jina lake Samueli, akisema, "Kwa maana nimemwomba kutoka kwa Bwana."
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
1 SAMUELI 2:1, 4—5, 6—7, 8abcd (K.1a)
K. Moyo wangu wamshangilia Bwana, Mwokozi wangu.
Moyo wangu wamtukuza Bwana;
na pembe yangu imetukuka katika Mungu wangu.
Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu,
kwa maana naufurahia wokovu wako. K.
Upinde wa mashujaa umevunjika,
bali walio dhaifu wamefungiwa nguvu.
Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula,
na hao waliokuwa na njaa wamepata raha.
Mwanamke tasa amezaa watoto saba,
naye mama wa wana wengi amefifia. K.
Ndiye Bwana anayeua, na anayehuisha,
hushusha hata kuzimu, tena huleta juu.
Bwana hufukarisha mtu naye hutajirisha,
hushusha chini, tena huinua juu. K.
Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
humpandisha mhitaji kutoka jaani,
ili awaketishe pamoja na wakuu,
wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu. K.
SHANGILIO LA INJILI
1 Wathesalonike 2:13
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Lipokeeni neno la Mungu, sio kama neno la wanad, bali kama lilivyo, yaani neno la Mungu.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 1:21b—28
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Wakati ule: Yesu aliingia katika sinagogi ya Kapernaumu, akafundisha siku ya Sabato. Watu walistaajabia mafundisho yake, kwa maana aliwafundisha kama mtu mwenye mamlaka na si kama Waandishi. Ndani ya sinagogi lao alikuwapo mtu amepagawa na pepo mchafu, akapaza sauti akisema, "Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Nakujua u nani, ndiwe Mtakatifu wa Mungu!" Yesu akamkemea akisema, "Nyamaza! Umtoke!" Pepo mchafu akamtikisatikisa, akamtoka huku akigumia kwa sauti kubwa. Wote wakashangaa na wakaulizana, "Kitu gani hiki? Haya ndiyo mafundisho mapya kwa mamlaka. Anawaamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii." Na sifa yake ikaenea katika ujirani wote wa Galilaya.
Injili ya Bwana.