SOMO LA KWANZA
Isaya 60:1—6
Somo katika kitabu cha Nabii Isaya
Amka! Uangaze, ewe Yerusalemu, kwa kuwa nuru yako imekuja, nao utukufu wa BWANA umekaa juu yako. Tazama, giza limeifunika dunia, na giza kuu limeyafunika mataifa, lakini juu yako Bwana atatokea, nao utukufu wake utaonekana juu yako. Mataifa watatembea katika mwanga wako, nao wafalme katika weupe wa alfajiri yako. Inua macho, utazame pande zote; wote wamekusanyika, wanakujia — wana wako watakuja toka mbali, binti zako wanabebwa kiunoni. Kwa kuona hayo, utatiwa nuru, moyo wako utapendezwa nayo na kuona raha; maana mali ya nchi za ng'ambo ya bahari zitakujia, na utajiri wa mataifa utakujia kwa wingi. Makundi ya ngamia watakufunika, ngamia vijana wa Midiani na Efa. Watu wa Sheba watakuja, wakileta dhahabu na ubani, na kutangaza sifa za Bwana.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 72:2, 7—8, 10—11, 12—13 (K. tazama 11)
K. Mataifa yote ya ulimwengu watakusujudia, ee Bwana.
EE Mungu, umpe mfalme hukumu yako;
na mwana wa mfalme haki yako;
ahukumu taifa lako kwa haki,
na wanyonge kwa usawa. K.
Katika siku zake haki iendelee,
na amani izidi mpaka mwezi ukome.
Atawale toka bahari hata bahari,
na toka ule mto hata miisho ya dunia. K.
Wafalme wa Tarshishi na visiwa watatoa kodi,
wafalme wa Sheba na Seba wataleta zawadi.
Wafalme wote wa dunia watamwangukia,
mataifa yote watamtumikia. K.
Maana atamkomboa maskini mwenye kumlilia,
na mnyonge asiye msaidizi.
Atamhurumia dhaifu na mhitaji,
na anayaokoa maisha ya wahitaji. K.
SOMO LA PILI
Waefeso 3:2—3a, 5—6
Somo katika barua ya Mtakatifu Paulo kwa Waefeso
Ndugu: Nadhani mmesikia jinsi Mungu alivyonikabidhi neema ya kuwasaidia ninyi, yaani kwa kunifunulia ujuzi wa fumbo. Kwa wazee wa zamani fumbo hilo halikujulikana kama lilivyofunuliwa sasa na Roho kwa mitume na manabii wake watakatifu. Maana sasa watu wa mataifa hurithi pamoja nasi, pia ni viungo vya mwili mmoja nasi, na wanashiriki ahadi moja nasi katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.
Neno la Bwana.
SHANGILIO LA INJILI
MATHAYO 2:2
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Tuliona nyota yake mashariki. Tumekuja kumwabudu Bwana.
W. Aleluya.
INJILI
Mathayo 2:1—12
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo
Yesu alipozaliwa Bethlehemu ya Yudea wakati wa mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, "Yuko wapi aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliona nyota yake mashariki. Tumekuja kumwabudu." Mfalme Herode aliposikia hayo, alihangaika sana, na Yerusalemu yote pamoja naye. Akawakusanya makuhani na Waandishi wote wa watu, akawauliza mahali pa kuzaliwa Kristo. Nao wakamwambia, "Bethlehemu ya Yudea, kwa maana nabii ameandika hivi: 'Ee Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, huwi kamwe mji wa mwisho kati ya miji mikubwa ya Yuda, kwa maana kwako atatokea kiongozi atakayewachunga watu wangu israeli.'" Hapo Herode akawaita mamajusi kwa faragha, akawahoji kuhusu wakati nyota ile ilipotokea. Akawatuma waende Bethlehemu akisema, "Nendeni mkapeleleze kwa bidii habari za mtoto. Mkimkuta, nipasheni habari, ili nami pia niende nikamwabudu." Walimsikiliza mfalme, wakaenda. Na tazama, nyota ile waliyoiona katika nchi ya mashariki ikawatangulia tena, hata ilipofika ikasimama juu ya mahali alipokuwapo mtoto. Walipoiona tena nyota, walifurahi kwa furaha kubwa sana. Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Maria mama yake. Wakaanguka, wakamwabudu. Wakafungua hazina zao wakamtolea zawadi za dhahabu, ubani na manemane. Wakiisha kuonywa katika ndoto wasimrudie Herode, wakarudi nchini kwao kwa njia nyingine.
Injili ya Bwana.