MASOMO YA MISA, IJUMAA YA JUMA LA KUMI NA SITA
KIPINDI CHA KAWAIDA, MWAKA II
KUMBUKUMBU YA WAT. YOAKIMU NA ANA, WAZAZI WA BIKIRA MARIA, JULAI 26, 2024
RANGI YA KILITURJIA: NYEUPE 🤍
SOMO LA KWANZA
YEREMIA 3:14—17
Nitawapa wachungaji wapendezao moyo wangu, nayo mataija yote watakusanyika huko Yerusalemu.
Somo katika kitabu cha Nabii Yeremia
Rudini, enyi wana waasi, asema Bwana, kwa maana ni mimi niliye Bwana wenu: nitamtwaa mtu mmoja wa mji, mmoja na wawili wa ukoo mmoja, na kuwarudisha kukaa Sioni. Hapo nitawapa wachungaji wapendezao moyo wangu, nao watawachunga kwa hekima na utaratibu. Ndipo mtakapoongezeka na kuwa wengi katika nchi asema Bwana, hawatasemna tena, "Sanduku agano la Bwana!" Hawatalifikiria tena, wala hawatalikumbuka, wala hawatalihitaji, wala hawataunda jingine jipya. Wakati ule wataita Yerusalemu, "Kiti cha enzi cha Bwana." Mataifa yote watakusanyika huko Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana, wala hawatafuata tena ukaidi wa mioyo yao mibaya.
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
YEREMIA 31:10, 11—12ab, 13 (K. tazama 10d)
K. Bwana atatulinda kama mchungaji alilindavyo kundi lake.
Enyi mataifa, lisikieni neno la Bwana,
litangazeni katika pwani za mbali.
Semeni: Aliyemtawanya Israeli atamkusanya;
atamlinda kama mchungaji alilindavyo kundi lake. K.
Kwa maana Bwana atamwokoa Yakobo,
atamwopoa katika mkono wa mtu mwenye nguvu kumpita yeye.
Watakuja na kupaza sauti kwa shangwe juu ya Mlima Sioni,
wataukimbilia wema wa Bwana. K.
Hapo binti watafurahi kwa kucheza ngoma,
na vijana na wazee vile vile.
Nitaigeuza huzuni yao kuwa changamko,
nitawatuliza na kuwafurahisha baada ya mateso yao. K.
SHANGILIO LA INJILI
TAZAMA LUKA 8:15
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Heri wenye kulisikia neno na kulishika kwa moyo dhahiri na mwema, wakazaa matunda kwa uvumilivu.
W. Aleluya.
SOMO LA INJILI
MATHAYO 13:18—23
Mwenye kulisikia neno na kulielewa, huyo huzaa matunda.
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo
Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake, "Haya! Ninyi usikilizeni mfano wa mpanzi. Mtu akilisikia neno la ufalme asilitunze moyoni, mwovu anamjia, akayanyang'anya yaliyopandwa moyoni mwake. Kwake, mbegu imeanguka kando ya njia. Mbegu imeanguka kwenye changarawe, ni mfano wa mtu anayelisikia neno, akalipokea mara kwa furaha. Lakini hana mizizi ndani yake. Basi hadumu. Panapotokea upinzani au madhulumu kwa ajili ya neno, anakwama mara. Mbegu imeanguka kati ya miba, ni mfano wa mtu anayelisikia neno, lakini shughuli za dunia na ulaghai wa mali hulisonga neno. Naye hatoi mavuno. Mbegu imeanguka katika udongo wenye
rutuba, ni mfano wa mtu anayelisikia neno na kulitunza moyoni. Akazaa na kutoa matunda: huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini."
INJILI YA BWANA... SIFA KWAKO EE KRISTO