SOMO LA KWANZA
Yeremia 17:5—10
Somo katika kitabu cha Nabii Yeremia
Bwana asema hivi: Ole wake mtu anayemtumainia mwanadamu, aliyemfanya mtu kuwa tegemeo lake, nao moyo wake umemwacha Bwana. Atakuwa kama kichaka mbugani, hataona heri hata kidogo; atakaa mahali pa joto, jangwani, katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Heri mtu anayemwaminia Bwana; aliyeweka matumaini yake katika Bwana. Atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, uenezao mizizi yake penye mto; wala hauogopi wakati wa hari unapofika, nayo majani yake yanazidi kuwa mabichi; wala hauhangaiki katika mwaka wa ukavu, wala hauachi kuzaa matunda. Moyo ni mdanganyifu kuliko vyote, ni mgonjwa hata usiweze kupona; nani awezaye kuujua? Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navipima viuno, ili kumlipa mtu kadiri ya njia zake, na kadiri ya mazao ya matendo yake.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 1:1—2, 3, 4 na 6 (Zaburi 40:5a)
K. Heri mtu anayemwaminia Bwana.
Heri mtu yule asiyefuata shauri la waovu,
asiyesimama katika njia ya wakosefu,
wala kukaa katika baraza la wenye mzaha.
Bali, furaha yake ni katika sheria ya Bwana,
na kuitafakari sheria yake mchana na usiku. K.
Naye ni kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Unaozaa matunda kwa wakati wake;
wala majani yake halinyauki,
na kila afanyalo linafanikiwa. K.
Sivyo walivyo waovu!
Wao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kwa maana Bwana anatunza njia ya waadilifu,
lakini njia ya waovu itapotea. K.
SHANGILIO LA INJILI
Luka 8:15
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
K. Wana heri wale wenye kulisikia neno na kulishika kwa moyo mkarimu na mwema, wakazaa matunda kwa uvumilivu.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
INJILI
Luka 16:19—31
Somo katika Injili ilivyoandikwa na Luka.
Wakati ule: Yesu aliwaambia Mafarisayo, "Palikuwa na mtu tajiri, aliyezoea kuvaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi na alijifurahisha kwa kufanya sherehe siku kwa siku. Mlangoni pake alilala maskini, jina lake Lazaro, aliyejaa vidonda. Alitamani kushibishwa walau makombo yaliyoanguka kutoka meza ya tajiri. Wakaja pia mbwa, wakamlamba vidonda vyake. Siku moja maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Abrahamu. Kisha tajiri akafa, akazikwa, na katika na katika mateso yake Jehanamu, aliyainua macho, akamwona Abrahamu kwa mbali, na Lazaro kifuani pake. Akapaza sauti, akalia, 'Baba Abrahamu, unihurumie. Umtume Lazaro achovye ncha ya kidole kwenye maji, apoze ulimi wangu, kwa maana nateswa sana katika moto huu.' Abrahamu akajibu, 'Mwana, kumbuka ya kuwa wewe ulipokea mema yako wakati wa maisha yako duniani, bali Lazaro vivyo alipatwa na mabaya; sasa huyu anatulizwa, bali wewe unateswa. Na juu ya hayo, kuna shimo kubwa kati yetu na yenu, hata kama watu wangetaka kuvukia kwenu, hawawezi, wala wa kwenu hawawezi kuvukia kwetu.' Akasema, 'Basi, baba, ninakukuomba umtume Lazaro aende katika nyumba ya baba yangu, maana nina ndugu watano, awaonye, wasije wakafika pia mahali hapa pa mateso.' Lakini Abrahamu akasema, 'Wanao Musa na manabii. Wawasikilize hao.' Yeye akasema, 'Sivyo, babae Abrahamu, bali mtu akienda kwao kutoka kwa wafu, watatubu.' Yeye lakini akajibu, 'Wasipowasikiliza Musa na manabii, hawatapokea hatae ushuhuda wa mtu aliyefufuka katika wafu.'"
Injili ya Bwana.