SOMO LA KWANZA
Yeremia 18:18—20
Somo katika kitabu cha Nabii Yeremia
Maadui wa Nabii walisema, "Njoni tupange njama dhidi ya Yeremia, kwani sheria haipotei kwa kumkosa kuhani, wala shauri halipotei kwa wenye hekima, wala neno halikosekani kwa nabii. Njoni tumpige kwa ulimi wetu, wala tusitilie maanani maneno yake yoyote." Nitegee sikio, ee Bwana, ukasikilize wayasemayo maadui zangu. Je, hurudisha mabaya kwa mema hata wanichimbie shimo wapoteze uzima wangu? Kumbuka kama nimesimama mbele yako, ili niwasemee mema, na kuepusha hasira yako mbali nao.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 31:5—6, 14, 15—16 (K. 17b)
K. Utuokoe, ee Bwana, kwa huruma ya upendo wako.
Unitoe kutoka wavu walionitegea,
maana wewe ndiwe kimbilio langu.
Mikononi mwako naiweka roho yangu;
Utaniokoa, ee Bwana, Mungu wa ukweli. K.
Nimesikia masingizio ya wengi,
vitisho vimenizunguka pande zote.
Wamepatana juu yangu,
wamekula njama kuuondoa uhai wangu. K.
Mimi lakini nakutumainia, ee Bwana,
nasema, "Wewe ndiwe Mungu wangu."
Maisha yangu yamo mikononi mwako,
Uniokoe na maadui zangu,
na mikono ya wadhulumu wangu. K.
SHANGILIO LA INJILI
Yohane 8:12
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
K. Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu, anifuataye mimi atakuwa na mwanga wa uzima.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo
INJILI
Mathayo 20:17—28
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Wakati ule: Yesu alipanda kwenda Yerusalemu. Njiani aliwakusanya wale Kumi na Wawili, akawaambia, "Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu. Huko Mwana wa Mtu atatiwa mikononi mwa makuhani wakuu na Waandishi, nao watamhukumu afe. Kisha watamtia mikononi mwa watu wa mataifa, ili wamdhihaki, wampige mijeledi na kumsulibisha. Na siku ya tatu atafufuka." Wakati ule, mama wa wana wa Zebedayo alimwendea pamoja na wanawe, akamsujudia amwombe neno. Akamwuliza, "Unataka nini?" Akamwambia, "Sema kwamba hawa wanangu wawili waketi, mmoja mkono wako wa kuume na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako." Yesu akajibu, "Hamjui mnayoyaomba. Je, mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi?" Wakajibu, "Twaweza." Akawaambia, "Vema, mtakinywea kikombe changu. Lakini kuketisha watu kuume au kushoto kwangu si mamlaka yangu, bali watapewa wale waliojaliwa na Baba yangu." Wale kumi wengine waliposikia hayo, waliona chuki juu ya ndugu hao wawili. Lakini Yesu aliwaita, akasema, "Mwajua ya kuwa watawala wa mataifa hupiga ubwana juu ya raia wao, na masultani huwatumikisha. Lakini kwenu isiwe hivyo, bali apendaye kuwa mkubwa wenu, awe mtumishi wenu; na apendaye kuwa wa kwanza wenu, awe mtumishi wenu. Kadhalika, Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumikia, na kutoa uhai wake kufidia wengi."
Injili ya Bwana.