SOMO LA KWANZA
Isaya 1:10, 16—20
Somo katika kitabu cha Nabii Isaya.
Sikilizeni neno la Bwana, enyi watawala wa Sodoma! Jiosheni, jitakaseni! Ondoeni uovu wa matendo yenu, usiwe tena mbele ya macho yangu; acheni kufanya mabaya, jifunzeni kutenda mema. Tafuteni yaliyo haki, msaidieni yule anayedhulumiwa, mpatieni yatima haki yake, mteteeni mjane. Njoni, tuongee, asema Bwana: Hata dhambi zenu zikiwa kama nguo nyekundu, zitageuka kuwa nyeupe kama theluji; hata zikiwa nyekundu kama damu, zitageuka kuwa kama sufu. Mkikubali kutii, mtakula mema ya nchi; bali, mkikataa na kuasi, mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya!
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 50:8—9, 16bc—17, 21 na 23 (K. 23b)
K. Yeye ambaye njia yake ni adili, nitamwonyesha wokovu wa Mungu.
Sikukaripii kwa ajili ya matoleo yako,
Sadaka zako za kuteketeza zipo mbele yangu daima.
Sitapokea fahali kutoka mashambani mwako,
Wala beberu kutoka kwenye mazizi yako. K.
Unawezaje kuzikariri sheria zangu,
Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
Wewe unayeyadharau maonyo,
Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako! K.
Unafanya haya, nami ninyamaze?
Unadhani ya kuwa mimi ni kama wewe?
Ninakushitaki: ninayaweka mashtaka hayo mbele yako.
Sadaka ya sifa, ndiyo inayonipa heshima;
Naye ambaye mwenendo wake hauna hatia,
Nitamwonyesha wokovu wa Mungu. K.
SHANGILIO LA INJILI
Ezekieli 18:31
K. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
K. Yatupilieni mbali maovu yote mliyofanya, ndilo neno la Bwana Mungu, na mjifanyie moyo na roho mpya.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
INJILI
Mathayo 23:1—12
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Wakati ule: Yesu aliwafundisha umati na wafuasi wake akisema, "Katika kiti cha Musa wameketi Waandishi na Mafarisayo. Kwa hiyo fanyeni na kushika yote wawaambiayo. Lakini matendo yao msiyaige, kwa maana wanasema lakini hawafanyi hivyo. Hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani, lakini wenyewe hawataki kuisogeza hata kwa kidole. Matendo yao yote huyafanya ili kutazamwa na watu. Kwa hiyo hutanua hirizi na kuongeza matamvua. Wanapenda nafasi za kwanza karamuni na viti vya mbele katika masinagogi, pia kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu 'Rabbi.' Bali ninyi msiitwe "Rabbi," maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu 'baba' duniani, maana Baba yenu ni mmoja ndiye aliye mbinguni. Wala msikubali kuitwa 'Waalimu' maana mwalimu wenu ni mmoja naye ndiye Kristo. Aliye mkubwa miongoni mwenu ni mtumishi wenu. Kila anayejikweza atanyenyekeshwa, na kila ajinyenyekeshaye atakwezwa."
Injili ya Bwana.