SOMO LA KWANZA
Danieli 9:4–10
Somo katika kitabu cha Danieli.
Ee Bwana, Mungu mkuu na wa ajabu, wewe washika agano na huruma kwa wale wanaokupenda na kushika amri zako! Sisi tumetenda dhambi, tumefanya maovu; tumekuwa wapotevu, tumeasi, na kuacha amri zako na maagizo yako. Wala hatukuwasikiliza watumishi wako manabii, walionena kwa jina lako mbele ya wafalme wetu, wakuu wetu nae baba zetu, na mbele ya taifa zima la nchi. Wewe, ee Bwana, ni mwenye haki; nasi tunaona aibu usoni mwetu; hata siku ya leo, watu wa Yuda, wenyeji wa Yerusalemu na wa Israeli nzima, wale walio karibu na walio mbali, katika nchi zote ulikowatawanya, kwa sababu ya makosa waliyokukosea. Ee Bwana, sisi tunaona aibu usoni, nao wafalme wetu, wakuu wetu na baba zetu, kwa sababu tumefanya dhambi mbele yako. Huruma na maondoleo ni kwa Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha manabii, watumishi wako.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 79:8–9, 11, 13
Ee Bwana, usitutende kadiri ya dhambi zetu.
Usiyakumbuke makosa ya baba zetu;
huruma yako itufikie hima, / kwani tumetaabika sana. K.
Utusaidie, ee Mungu wokovu wetu,
kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
Utuokoe, utusamehe dhambi zetu,/ kwa ajili ya jina lako. K.
Lakini sisi, watu wako na kondoo za malisho yako,
tutakutolea shukrani zetu sasa na milele;
tutatangaza sifa zako kizazi kwa kizazi. K.
SHANGILIO LA INJILI
Yohane 6:63c, 68c
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
K. Maneno yako, ee Bwana, ni roho tena ni uzima, wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
INJILI
Luka 6:36—38
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Luka
Wakati ule: Yesu aliwaambia wanafunzi wake, "Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa. Msipatilize, nanyi hamtapatilizwa. Sameheni, nanyi mtasamehewa. Toeni, nanyi mtapewa; kipimo chema kilichoshindiliwa, kutikiswa na kujazwa hata kumwagika, watawatilia pindoni mwenu. Kwa maana kipimo mnachopimia mtapimiwa.
Injili ya Bwana.