SOMO LA KWANZA
Kumbukumbu La Torati 26:16—19
Somo katika kitabu cha Kumbumbu la Torati.
Musa alinena na watu, akawaambia: "Bwana Mungu wako anakuamuru leo uzitende sheria na kawaida hizo. Utazishika na kuzitenda kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote. Leo umekubali kwamba Bwana ndiye Mungu wako: yakupasa utembee katika njia zake na kushika kanuni zake, amri zake na kawaida zake na kusikiliza sauti yake. Naye Bwana amekuungama leo kwamba: utakuwa taifa lake la pekee jinsi alivyokuambia kwa kuwa yakupasa ushike amri zake, naye atakuinua juu ya mataifa yote aliyoyafanya, kwa heshima, sifa na utukufu, nawe utakuwa taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako, jinsi alivyokuahidi."
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 119:1—2, 4—5, 7—8
K. Heri waendao katika sheria ya Bwana.
Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya Bwana.
Heri wazishikao shuhuda za Mungu,
Wanaomtafuta Bwana kwa moyo wao wote. K
Wewe umewaamuru, wazishike kanuni zako kwa uangalifu.
Naam, heri njia zangu zingekuwa thabiti,
Ili nizitii amri zako! K
Nitakusifu kwa moyo mnyofu,
Nikijifunza hukumu zako za haki.
Kanuni zako nitazifuata,
Usiniache peke yangu!
SHANGILIO LA INJILI
Amo 5:14
K. Sifa na utukufu kwako Ee Kristo
Kumbe, Sasa ndio wakati wa neema; tazama, Sasa, ndio siku ya wokovu.
W. Sifa na utukufu kwako Ee Kristo.
INJILI
Mathayo 5:43—48
SOMO la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Wakati ule: Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako.' Mimi lakini nawaambieni: Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowadhulumu ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua waadilifu na wasio waadilifu. Mkiwapenda wale tu wawapendao ninyi, mwapata tuzo gani? Je, watoza ushuru hawafanyi vile? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnazidi nini? Je, wapagani hawafanyi vile vile? Basi, muwe wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu."
Injili ya Bwana.