SOMO LA KWANZA
Ezekieli 18:21—28
Somo katika kitabu cha Nabii Ezekieli.
Bwana Mungu asema hivi: Mtu mwovu akiacha dhambi zake alizofanya, akishika amri zangu zote na kutenda yaliyo haki na sawa, ataishi, wala hatakufa! Hata moja ya dhambi zake alizofanya, haitakumbukwa juu yake; ataishi kwa sababu ya haki aliyotenda. Je, mimi nataka kufa kwake mtu mwovu? Asema Bwana Mungu. Sio zaidi aache njia zake mbaya ili apate kuishi? Lakini mtu wa haki akiacha haki yake na kutenda maovu, akifanya machukizo yote kama mtu mwovu anavyofanya, je, ataishi? Hata moja ya matendo ya haki aliyofanya, halitakumbukwa; kwa sababu ya kosa lile alilokosa na dhambi ile aliyofanya, kwa sababu hiyo atakufa. Lakini ninyi mwasema, “Njia ya Bwana si sawa!” Sikilizeni sasa, enyi watu wa nyumba ya Israeli: Je, njia yangu si sawa? Si zaidi njia zenu zisizo sawa? Mtu wa haki akiacha haki yake, na kutenda maovu na kufa, anakufa sababu ya uovu aliofanya. Na mtu mwovu akiacha uovu aliotenda na kufanya yaliyo haki na sawa, yeye atajipatia uzima; ameacha makosa yote aliyokosa, hakika ataishi; wala hatakufa.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 130:1—2, 3—4, 5-6, 7—8 (K. 3)
K. Kama wewe, ee Bwana,
Ungeyahesabu maovu yetu, nani angesimama?
Toka vilindini nakulilia, ee Bwana;
Ee Bwana, isikie sauti yangu!
Masikio yako na yasikilize
Sauti ya maombi yangu. K.
Kama wewe, ee Bwana ungeweka
Kumbukumbu ya dhambi zetu
Ee Bwana, nani angesimama?
Lakini kwako kuna msamaha,
Ili wakutumikie kwa uchaji. K.
Ninamngoja Bwana, roho yangu inamngoja,
Na ninalitumainia neno lake.
Roho yangu inamngoja Bwana,
Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi. K.
Ee Israeli, umngoje Bwana.
Kwa maana kwa Bwana kuna fadhili,
Kwake kuna wokovu mwingi.
Yeye ataiokoa Israeli/ na maovu yake yote. K.
SHANGILIO LA INJILI
Ezekieli 18:31
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
K. Yatupilieni mbali makosa yote mliyoyafanya,
Asema Bwana, mjifanyizie moyo mpya na roho mpya.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
INJILI
Mathayo 5:20—26
Somo katika Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Wakati ule: Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Uadilifu wenu usipozidi ule wa Waandishi na wa Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Mmesikia ya kuwa watu wa kale waliambiwa ‘ Usiue; na mtu akiua, astahili kushtakiwa.” Mimi nawaambieni, hata mtu anayemkasirikia ndugu yake, anastahili kushtakiwa. Amwambiaye ndugu yake ‘Raka’, astahili kesi katika baraza kuu la wazee. Amwambiaye ‘Mjinga’, anastahili moto wa Jehanamu. Basi ukipeleka sadaka yako kwenye altare, na hapo ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno na wewe, iache sadaka yako hapo mbele ya altare, nenda kwanza ukapatane na ndugu yako. Kisha rudi kutoa sadaka yako. Usikawie kupatana na mshitaki wako uwapo bado njiani naye, asije akakutoa kwa hakimu, na hakimu akutoe kwa tayarishi, naye akakutupa gerezani. Amin, nakuambia, humo hutoki tena hadi uwe umelipa senti ya mwisho.
Injili ya Bwana.