SOMO LA KWANZA
1 Petro 5:1—4
Somo katika barua ya kwanza ya Mtakatifu Petro.
Wapendwa: Enyi wazee, mimi niliye mzee mwenzenu na shahidi wa mateso ya Kristo na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye, nawasihi: lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa na kulitunza, sio kwa sababu ni wajibu wenu, bali kwa furaha kama Mungu atakavyo; wala sio kwa ajili ya kujipatia faida chafu, bali kwa bidii ya moyo. Msijifanye mabwana kwa makundi yaliyowekwa katika uchungaji wenu, bali muwe mifano kwa kundi zima. Na mchungaji mkuu atakapotokea mtapokea taji la utukufu isiofifia.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 23:1—3a, 3b—4, 5, 6 (K. 1)
K. Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu.
Bwana ndiye mchungaji wangu,
sitapungukiwa na kitu.
Hunipumzisha katika malisho mabichi;
hunipeleka kwenye maji matulivu; hunipatia nguvu. K.
Huniongoza katika njia zilizo sawa / kwa ajili ya jina lake.
Hata nijapopita katika bonde la giza,
siogopi mabaya, kwani wewe upo pamoja nami;
gongo lako na fimbo yako vyanituliza. K.
Waandaa meza mbele yangu,
machoni pa adui zangu;
umenipaka mafuta kichwani;
kikombe changu kinafurika. K.
Kweli, wema na fadhili zitanifuata
siku zote za maisha yangu.
Nitakaa nyumbani mwa Bwana
kwa miaka mingi ijayo. K.
SHANGILIO LA INJILI
MATHAYO 16:18
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
K. Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, na milango ya Jehanamu haitalishinda.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
INJILI
Mathayo 16:13—19
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Wakati ule:Yesu aliingia sehemu ya Kaisaria Filipi. Akawauliza wafuasi wake, "Watu wanasema Mwana wa Mtu ni nani?" Wakasema, "Wengine Yohane Mbatizaji, wengine, Eliya, tena wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii." Akawaambia, "Na ninyi mwasema kuwa mimi ni nani?" Simoni Petro akajibu, "Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai." Yesu akamjibu, " Mwenye heri wewe Simoni, mwana wa Yona, kwa maana si mwili na damu vilivyokufunulia hayo, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu, na milango ya Jehanamu haitalishinda. Na wewe nitakupa funguo za ufalme wa mbingu. Lolote utakalofunga duniani, litafungwa mbinguni pia; na lolote utakalofungua duniani, litafunguliwa pia."
Injili ya Bwana