SOMO LA KWANZA
Yona 3:1—10
Somo katika kitabu cha Nabii Yona
Hapo neno la Bwana lilimjia Yona: Simama, nenda Ninawi, ule mji mkubwa, ukautangazie niliyokuamuru. Yona akasimama akaenda Ninawi kwa amri ya Bwana. Basi, Ninawi ulikuwa mji mkubwa mbele ya Mungu, ukubwa wake ulikuwa mwendo wa siku tatu. Alipokwishaingia mjini mwendo wa siku moja, Yona alianza kuhubiri, akisema, "Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamia." Watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu, wakautangaza mfungo kwa wakubwa na wadogo, wakavaa magunia. Habari ilimfikia hata mfalme wa Ninawi; naye akainuka mara katika kiti chake cha enzi, akayavua mavazi yake ya kifalme, akalivaa gunia na kuketi juu ya majivu. Pia akatangaza katika Ninawi yote kwa amri ya mfalme na wakuu wake: "Mtu wala mnyama asile chochote, wala ng'ombe wala kondoo, wasile chakula wala wasinywe maji. Watu na wanyama wavae magunia: wamlilie Mungu kwa nguvu. Kila mmoja auache mwenendo wake mbaya na uovu wa mikono yake. Nani ajuaye huenda Mungu akafikiri bado na kujuta; labda ataiacha hasira yake kali; hata tusiangamie?" Mungu alipoona waliyoyafanya jinsi walivyoacha mwenendo wao mbaya, aliwaonea huruma akaacha kuleta uharibifu aliotangaza kwamba atauleta.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 51:1—2, 10—11, 16—17
K. Moyo uliovunjika na mnyenyekevu, ee Mungu, hutaudharau.
Unihurumie, ee Mungu, kulingana na wema wako;
Kwa kadiri ya huruma yako kuu, uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu;
unitakase dhambi yangu. K.
Uniumbie moyo safi, ee Mungu;
Ufanye upya roho thabiti ndani yangu.
Usinitupe mbali na uso wako,
wala usiniondolee roho yako takatifu. K.
Kwa maana hupendezwi na sadaka, la ningalikutolea;
wewe hupokei sadaka ya kuteketezwa.
Sadaka ya Mungu ni roho iliyovunjika;
moyo uliyovunjika na mnyenyekevu, ee Mungu, hutaudharau. K.
SHANGILIO LA INJILI
Yoeli 2:12—13
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo
K. Hata sasa, asema Bwana, mnirudie kwa mioyo yenu yote,
Kwa maana mimi ni mpole na mwenye huruma.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
INJILI
Luka 11:29—32
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Luka
Wakati ule: Makundi ya watu yalipokusanyika, Yesu alisema, "Kizazi hiki ni kizazi kiovu; chatamani ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote, ila ishara ya Yona. Maana kama Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo Mwana wa Mtu atakavyokuwa ishara kwa kizazi hiki. Siku ya hukumu malkia wa kusini atasimama na watu wa kizazi hiki na kuwahukumu, kwa maana yeye alikuja kutoka miisho ya dunia asikie hekima ya suleimani, na hapa yupo aliye mkubwa kuliko Suleimani. Siku ya hukumu watu wa Ninawi watasimama na kizazi hiki na kukihukumu, kwa maana walitubu alipohubiri Yona. Tazama, hapa yupo yeye aliye mkubwa kuliko Yona."
Injili ya Bwana.