SOMO LA KWANZA
Isaya 55:10—11
Somo katika kitabu cha Nabii Isaya
Bwana asema hivi: Kama vile mvua na theluji zishukavyo kutoka mbinguni, wala hazirudi huko bila kuinywesha ardhi na kuizalisha na kuichipusha, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula, vivyo hivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 34:3—6, 15—18
K. Bwana anawaokoa wanyofu katika shida zao zote.
Mtukuzeni Bwana pamoja nami,/ tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nikimkimbilia Bwana, akanisikiliza,
akaniopoa katika hofu zangu zote. K.
Mtazameni Mungu mkafurahi, / na nyuso zenu zisihuzunike.
Maskini huyu alilia, Bwana akamsikiliza,
Akamwokoa katika shida zake zote. K.
Macho ya Bwana yawaangalia wenye haki
na masikio yake hukielekea kilio chao.
Uso wa Bwana ni juu ya watendao mabaya,
ili afute kumbukumbu ya duniani. K.
Wanyofu waliita Bwana akasikia,
Akawaopoa katika shida zao zote.
Bwana yu karibu nao waliopondeka moyo,
huwaokoa wenye kuvunjika moyo. K.
SHANGILIO LA INJILI
Mathayo 4:4b
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
K. Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo kinywani mwa Mungu.
W. Sifa na utukufu kwako ee Kristo.
INJILI
Mathayo 6:7—15
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo
Wakati ule: Yesu aliwaambia wanafunzi wake, "Katika sala zenu msipige makelele mengi kama wapagani. Hao wanadhani kwamba watasikilizwa wakitamka maneno mengi. Msiwaige, maana Baba yenu anajua mahitaji yenu hata kabla hamjamwomba. Basi, ninyi salini hivi: Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako ufike, utakalo lifanyike, duniani kama huko mbinguni. Utupe leo mkate wetu wa kila siku; Utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea; usitutie katika kishawishi, lakini utuopoe maovuni. Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu."
Injili ya Bwana.