SOMO LA KWANZA
Mambo Ya Walawi 19:1—2, 11—18
Somo katika kitabu cha Mambo ya Walawi
Bwana alinena na Musa, akamwambia: Sema na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Muwe watakatifu, kwa maana mimi, Bwana Mungu wenu, ni mtakatifu. Hata mmoja wenu asiibe, asiseme uwongo wala asimdanganye mwenziwe. Msiape uwongo kwa jina langu; hivyo kulikufuru jina la Mungu wako. Ndimi Bwana. Usimdhulumu mwenzako, wala usimnyang’anye; mshahara wa mtu wa kazi usilale kwako mpaka kesho asubuhi. Usimlaani kiziwi, wala usiweke kwazo mbele ya kipofu, bali umheshimu Mungu wako. Ndimi Bwana. Msitende yasiyo haki katika hukumu. usimpendelee aliye mdogo mtu wala usimheshimu mno mwenye cheo; bali jirani yako utamhukumu kwa haki. Usizunguke kuwachongea jirani zako, wala usiponze damu ya jirani yako. Ndimi Bwana. Usiwe na chuki moyoni mwako kwa ndugu yako. Yakupasa kumkaripia jirani yako, ili usipatikane na kosa la dhambi. Usilipize kisasi, wala usiwaonee kinyongo wana wa kabila lako. Umpende jirani yako nafsi yako kama unavyojipenda mwenyewe. Ndimi Bwana.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 19:8, 9, 10, 15 (K. 6:63)
K. Maneno yako, ee Bwana, ni roho, tena ni uzima.
Sheria ya Bwana ni kamilifu,
yautuliza moyo.
Maagizo ya Bwana ni imara,
yanamletea mjinga hekima. K.
Maagizo ya Bwana ni ya haki,
yanaufurahisha moyo,
agizo la Bwana ni safi,
linayatia macho mwangaza. K.
Uchaji wa Bwana ni safi,
hudumu hata milele.
Hukumu za Bwana ni kweli,
zote ni za haki kamili. K.
Maneno ya kinywa changu yakupendeze wewe,
nayo mawazo ya moyo wangu, yaliyo mbele yako,
ee Bwana, Mwamba wangu na mkombozi wangu. K.
SHANGILIO LA INJILI
2 Wakorintho 6:2b
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
K. Kumbe, sasa ndio wakati uliokubalika;
tazama, sasa ndio siku ya wokovu.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
INJILI
Mathayo 25:31—46
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo
Wakati ule: Yesu aliwaambia wanafunzi wake, "Atakapokuja Mwana wa Mtu katika utukufu wake na malaika wote pamoja naye, ataketi katika kiti cha utukufu wake. Na mataifa yote watakusanywa mbele zake, atawabagua watu kama vile mchungaji anavyobagua kondoo na mbuzi. Atawaweka kondoo upande wake wa kuume, na mbuzi upande wake wa kushoto. Halafu mfalme atawaambia wale wa kuume kwake, 'Njoni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu. Urithini ufalme mliowekewa tangu mwanzo wa dunia. Kwa maana nalikuwa na njaa, mkanilisha, nalikuwa na kiu, mkaninywesha, nalikuwa mgeni, mkanikaribisha, nalikuwa uchi mkanivisha, nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama, nalikuwa kifungoni, mkaja kuniona.' Hapo waadilifu watamjibu na kusema, 'Bwana, lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvisha? Au lini tulikuona u mgonjwa au kifungoni, tukaja kukuona?' Mfalme atawajibu, 'Amin, nawaambieni, mliyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.' Kisha atawaambia na wale wa kushoto, 'Ondokeni kwangu ninyi walaaniwa, nendeni katika moto wa milele uliowekwa tayari kwa Shetani na malaika wake. Kwa maana nalikuwa na njaa, hamkunilisha; nalikuwa na kiu, hamkuninywesha. Nalikuwa mgeni, hamkunikaribisha; nalikuwa uchi, hamkunivisha; nalikuwa mgonjwa na kifungoni, msije hamkunitazama.' Hapo wao pia watajibu na kusema, 'Bwana, lini tulikuona una njaa, au una kiu, au mgeni, au huna nguo, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikutumikie?' Naye atawajibu, 'Amin, nawaambieni, mliyokosa kumtendea mmojawapo katika hawa wadogo, hamkunitendea mimi.' Na hao wataingia katika adhabu ya milele; bali waadilifu wataingia katika uzima wa milele."
Injili ya Bwana.