SOMO LA KWANZA
Mwanzo 9:8—15
Somo katika kitabu cha Mwanzo
Mungu alisema hivi na Nuhu na wanawe: "Mimi ninafunga agano langu nanyi, pia na vizazi vyenu baada yenu, tena na viumbe vyote vyenye uzima vilivyo pamoja nanyi: ndege, na wanyama wa kufugwa, wanyama wote wa mwitu walio pamoja nanyi, wote waliotoka katika safina, wanyama wote wa nchi. Nitaweka agano langu nanyi: hakuna kiumbe chenye mwili kitakachoangamizwa tena na gharika, wala hakutakuwako tena na gharika ya kuiharibu nchi. Mungu akasema: Hii ndiyo alama ya agano ninaloweka kati yangu mimi nanyi, na viumbe vyote vyenye uzima vilivyoko pamoja nanyi, kwa vizazi vijavyo: Nauweka upinde wangu wa mvua mawinguni, nao utakuwa alama ya agano kati yangu mimi na dunia. Nitakapoleta mawingu juu ya nchi, na huo upinde utakapoonekana mawinguni, nitalikumbuka agano lililo kati yangu mimi nanyi, na viumbe vyote vyenye uzima, yaani kila kilicho na mwili; wala maji hayatakuwa tena gharika ya kuharibu kila kiumbe chenye mwili."
Neno la Bwana .
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 25:4bc—5ab, 6—7ab, 8—9 (K. 10)
K. Mapito yako yote, ee Bwana, ni uaminifu na kweli kwa wale washikao agano lako.
au: Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli.
Ee BWANA, unionyeshe njia zako;
unijulishe mapito yako.
Uniongoze katika uaminifu wako, unifundishe,
maana wewe ndiwe Mungu mwokozi wangu. K.
Ee BWANA, ukumbuke huruma yako;
na rehema zako,
maana ni za tangu milele.
Unikumbuke kwa kadiri ya upendo wako. K.
Bwana ni mwema, tena mwenye haki,
kwa hiyo huwajulisha wakosefu njia zake.
Huwaongoza wanyenyekevu katika haki,
na kuwafundisha njia yake. K.
SOMO LA PILI
1 Petro 3:18—22
Somo katika barua ya kwanza ya Mtakatifu Petro
Wapendwa: Kristo alikufa mara moja kwa ajili ya dhambi. Mwadilifu alikufa kwa ajili ya wakosefu, ili awapeleke kwa Mungu. Aliuawa katika mwili, akahuishwa katika roho. Hivyo alikwenda kuhubiri kwa roho zilizokaa kifungoni. Zamani Nuhu alipounda safina, na Mungu alipongoja kwa subira, roho hizo zilikataa kusikiliza. Wachache tu, yaani, wanane, waliingia wakaokolewa katika maji. Maji hayo ni mfano wa ubatizo unaowaokoa ninyi sasa. Ubatizo si kuondoa uchafu wa mwili, bali ni kumwomba Mungu tupate dhamiri njema kwa nguvu ya ufufuko wa Yesu Kristo. Naye amewaweka malaika na wenye enzi na wenye nguvu chini ya mamlaka yake. Akaingia mbinguni. Yuko kuume kwa Mungu.
Neno la Bwana.
SHANGILIO LA INJILI
Mathayo 4:4b
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
K. Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo kinywani mwa Mungu.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
INJILI
Marko 1:12—15
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Wakati ule: Roho alimsukuma Yesu aende nyikani, na akakaa nyikani siku arobaini akijaribiwa na Shetani. Basi alikuwako pamoja na wanyama wa porini, na malaika walimtumikia. Baada ya Yohane kufungwa gerezani, Yesu alifika Galilaya akaihubiri Injili ya ufalme wa Mungu, akisema, "Wakati umefika, na ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini injili."
Injili ya Bwana