SOMO LA KWANZA
Isaya 58:9b—14
Somo katika kitabu cha Nabii Isaya
Bwana asema hivi: Ukiondoa nira isipatikane tena kwako, ukiacha na kidole cha kutisha, na maneno maovu; ukimpa mwenye njaa chakula chako, na kumshibisha mwenye kudhulumiwa; hapo mwanga wako utang'aa katika giza, na giza lako litageuka kuwa kama mchana; naye Bwana atakuongoza siku zote, katika jangwa atakushibisha. Atakurudishia nguvu zako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui. Nawe utajenga juu ya magofu ya kale; utainua misingi ya vizazi vingi; watakuita majina ya kupanga. "Mtengeneza mahali palipobomoka; mwenye kurejesha njia za haki." Kama ukiizuia miguu yako usiivunje Sabato, na usifanye anasa zako katika siku yangu takatifu; kama ukiita siku ya Sabato, furaha, na siku takatifu ya Bwana tukufu, na kama ukiitukuza kwa kutofanya mambo yako mwenyewe, wala kusema maneno yasiyofaa, ndipo basi utamfurahia Bwana, nami nitakuongoza kati ya shangwe, hata kwenye nchi iliyoinuka; nitakupa urithi wa Yakobo, baba yako. Kwa maana, kinywa cha Bwana kimenena hayo.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 86:1—2, 3—4, 5—6
K. Unifundishe, ee Bwana, njia yako,
nienende katika kweli yako.
Utege sikio lako, ee Bwana, unisikilize,
maana mimi ni mnyonge na maskini.
Uilinde nafsi yangu,maana mimi ni mchaji;
umwokoe mtumishi wako anayekutumaini. K.
U Mungu wangu; Unihurumie, ee Bwana,
kwa maana ninakulilia mchana kutwa.
Ufurahishe roho ya mtumishi wako;
kwako ee Bwana, nakuinulia roho yangu. K.
Kwa sababu wewe, ee Bwana, ni mwema na mpole,
umejaa huruma kwa wote wanaokuomba.
Usikie, ee Bwana, sala yangu;
uelekee sauti ya maombi yangu. K.
SHANGILIO LA INJILI
Ezekieli 33:11
K. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
W. Sikufurahii kufa kwake mtu mbaya, asema Bwana, bali nafurahia kuongoka kwake, apate kuishi.
K. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
INJILI
Luka 5:27—32
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Luka.
Wakati ule: Yesu alimwona mtoza ushuru, jina lake Lawi, ameketi forodhani, akamwambia, "Nifuate." Naye akaacha vyote, akasimama, akamfuata. Kisha Lawi akamwandalia karamu kubwa nyumbani kwake, na walikuwako na watoza ushuru wengi na watu wengine walioketi mezani pamoja nao. Mafarisayo na Waandishi wao wakanung'unika kwa wafuasi wake wakisema, "Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wakosefu?" Yesu akajibu, akawaambia, "Wenye afya hawahitaji tabibu, bali wagonjwa. Sikuja kuwaita waadilifu, bali wakosefu, wapate kutubu."
Injili ya Bwana.