SOMO LA KWANZA
Kumbukumbu La Torati 30:15—20
Somo katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati.
Musa alinena na watu, akawaambia, “Tazama, ninakuwekea leo mbele yako uzima na heri, mauti na uovu. Ukisikiliza amri za Bwana Mungu wako ninazokuamuru leo, na kumpenda Bwana Mungu wako, ukizifuata njia zake na kushika maagizo yake na amri zake na hukuma zake, utaishi na kuongezeka, Bwana Mungu wako atakubariki katika nchi unayoingia iwe yako. Lakini moyo wako ukigeuka usisikilize, ukivutwa na miungu mingine kuiabudu na kuitumikia, ninakuhakikishia leo utaangamia: hutaishi muda mrefu katika nchi unayokwenda kuimiliki uvukapo Yordani. Ninakushuhudishia mbingu na dunia: ninakuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka au laana. Chagua basi uzima uishi wewe na kizazi chako, kwa kumpenda Bwana Mungu wako, kwa kusikiliza sauti yake, na kuambatana naye. Kwa kuwa huo ndio uzima wako, na kudumu kwako muda mrefu katika nchi Bwana aliyowaapia kuwapa baba zako Abrahamu, Isaka na Yakobo.”
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 1:1-2, 3, 4 NA 6 (K. 40:5ab)
K. Heri mtu anayemtumainia Bwana.
Heri mtu Yule asiyefuata shauri la waovu,
asiyesimama katika njia ya wakosefu,
wala kukaa katika baraza la wenye mzaha.
Bali, furaha yake ni sheria ya Bwana,
na kuitafakari sheria yake mchana na usiku. K.
Naye ni kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
unaozaa matunda kwa wakati wake;
wala majani yake hayanyauki;
kila wafanyalo linafanikiwa. K.
Sivyo, walivyo waovu!
Wao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Maana Bwana anatunza njia yao waadilifu,
lakini njia ya waovu itapotea. K.
SHANGILIO LA INJILI
Mathayo 4:17
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
K. Tubuni, asema Bwana,
kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
INJILI
Luka 9:22-25
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Luka
Wakati ule: Yesu aliwaambia wanafunzi wake, akasema “Lazima Mwana wa Mtu kupatwa na mateso mengi, kukataliwa na wazee, pia na makuhani wakuu na Waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka.” Akawaambia wote, “Mtu akitaka kuwa mfuasi wangu, ajikane mwenyewe, lazima ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa maana mtu akitaka kuisalimisha nafsi yake ataipoteza, lakini mtu akiipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataikoa. Yamfaa mtu nini akipata dunia yote lakini kujipoteza au kujiangamiza mwenyewe?”
Injili ya Bwana.