SOMO LA KWANZA
Yoeli 2:12—18
Somo katika kitabu cha Nabii Yoeli
Bwana asema hivi: Mnirudie kwa moyo wenu wote, kwa kufunga, na kulia, na kuomboleza. Irarueni mioyo yenu, sio mavazi yenu, mrudieni Bwana, Mungu wenu, kwa maana yeye ni mpole na mwingi wa huruma, sio mwepesi wa hasira ni mwingi wa rehema, ni mwenye kuisikitikia taabu yenu. Ni nani anayejua? Labda, atarudi na kusikitika, na kuwaachia baraka yake. Mmtolee Bwana, Mungu wenu, matoleo na sadaka ya kinywaji. Pigeni baragumu katika Sioni, mtoleeni Mungu mafungo, tangazeni kusanyiko la ibada, kusanyeni watu wa taifa, muwaite katika mkutano mtakatifu, muwakutanishe wazee, muwakusanye watoto wachanga, nao wanyonyao maziwa. Bwana harusi atoke chumbani kwake, na bibi harusi katika kikao chake. Kati ya mlango wa hekalu na altare wale makuhani, walio watumishi wa Bwana, waseme: "Ee Bwana, ulihurumie taifa lako! Wala usitoe urithi wako upate aibu, na kuchekwa na mataifa. Kwanini katika mataifa waseme: 'Yuko wapi Mungu wao?'" Ndipo Bwana aliitendea nchi yake kwa moyo wa mapendo, akalihurumia taifa lake.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 51:1—4, 10—12, 15
K. Uturuhumie, ee Mungu, kwa kuwa tumetenda dhambi.
Unihurumie, ee Mungu, kulingana na wema wako;
kwa kadiri ya huruma yako kuu, uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu. K.
Kwa maana nayatambua makosa yangu,
na dhambi yangu ipo daima mbele yangu.
Nimekukosea wewe peke yako,
nikatenda yaliyo mabaya mbele za macho yako. K.
Uniumbie moyo safi, ee Mungu,
ufanye upya roho dhabiti ndani yangu.
Usinitupe mbali na uso wako,
wala usiniondolee roho yako takatifu. K.
Unirudishie furaha ya wokovu wako,
Unitegemeze kwa kunijalia roho sikivu.
Ee Bwana, ufumbue midomo yangu
na kinywa changu kitatangaza sifa zako. K.
SOMO LA PILI
2 Wakorintho 5:20—6:2
Somo katika barua ya pili ya Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho
Ndugu zangu: Tumekuwa wajumbe mahali pa Kristo, kwa maana ni Mungu anayeonya kwa huduma yetu. Na ombi tunalotoa kwa jina la Kristo ndilo hili: mpatanishwe na Mungu. Yeye amemfanya yule asiyejua dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili na sisi tuwe uadilifu wa Mungu katika yeye. Sisi tulio wafanyakazi pamoja na Mungu, tunawaonya msiipokee bure neema ya Mungu. Maana asema: "Wakati wa neema nawasikiliza; siku ya wokovu nawasaidia." Kumbe, sasa ndio wakati wa neema; sasa ndio siku ya wokovu.
Neno la Bwana.
SHANGILIO LA INJILI
Zaburi 95:7d, 8a
W. Sifa na utukufu kwako ee Kristo.
K. Ingekuwa heri leo msikie sauti ya Bwana, msiifanye migumu mioyo yenu.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
INJILI
Mathayo 6:1—6, 16—18
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo
Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake, "Angalieni, msifanye matendo yenu mbele ya watu, kusudi wawaone. Mkifanya hivyo, hamna thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi, unaposaidia wenye shida, usipige tarumbeta mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili wasifiwe na watu. Amin, nawaambieni, wamekwisha pata tuzo yao. Wewe unaposaidia wenye shida, hata mkono wako wa kushoto usilijue tendo la mkono wako wa kuume. Hivyo ufadhili wako uwe faraghani, na Baba yako aonaye faraghani atakutukuza. Kadhalika mnaposali, msiwe kama wanafiki. Hao wanaposali wapenda kusimama katika sinagogi na njia panda, ili waonekane na watu. Amin, nawaambieni, wamekwisha pata tuzo yao. Bali wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango wako, usali kwa Baba yako faraghani, na Baba yako aonaye faraghani atakutuza. Mnapofunga, msikunje nyuso kama wanafiki, maana hujiumbua nyuso, ili waonekane kwa watu wanafunga. Amin, nawaambieni, wamekwisha pata tuzo yao. Bali wewe unapofunga, ujipake mafuta kichwani, unawe uso, ili usionekane kwa watu unafunga, ila kwa Baba yako aliye faraghani; na Baba yako aonaye faraghani atakutuza."
Injili ya Bwana.