SOMO LA KWANZA
Yakobo 1:12—18
Somo katika barua ya Mtakatifu Yakobo
Ana heri mtu avumiliaye kishawishi, kwa maana akiwa amekishinda atapata taji la uzima alilowaahidia Mungu, wenye kumpenda. Mtu anaposhawishiwa asiseme, "Ninashawishiwa na Mungu." Maana Mungu hawezi kushawishi kutenda mabaya, wala yeye mwenyewe hamshawishi mtu. Kila mtu anashawishiwa akivutwa na kubembelezwa na tamaa yake mwenyewe. Na baada ya kuchukua mimba, tamaa inazaa dhambi, na dhambi inapokomaa inazaa mauti. Ndugu zangu wapendwa, msikubali kudanganywa. Kila kipaji chema na kila kipawa kamili hushuka kutoka juu kwa Baba wa mwanga, lakini kwake yeye mwenyewe hakuna ugeuzi wala kivuli cha ubadilifu. Kwa hiari yake ametuzaa kwa neno la ukweli, tupate kuwa kama limbuko la viumbe vyake.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 94:12—13a, 14—15, 18—19 (K. 12a)
K. Heri mtu yule unayemwadhibu, ee Bwana.
Heri mtu yule unayemwadhibu, ee Bwana,
na kumfundisha kwa sheria yako;
upate kumstarehesha siku za uovu. K.
Bwana hatalitupa taifa lako,
wala hutauacha urithi wako;
kwa hukumu itakuwa ya haki,
na wote wenye mioyo minyofu wataifuata. K.
Niliposema, "Mguu wangu umeteleza,"
fadhili zako, ee Bwana, zilinitegemeza.
Mashaka yalipoongezeka moyoni mwangu,
faraja zako ziliituliza roho yangu. K.
SHANGILIO LA INJILI
Yohane 14:23
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mtu akinipenda, atalishika neno langu, asema Bwana; na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 8:14–21
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Wakati ule: Wafuasi wake Yesu walisahau kuchukua mikate; na walikuwa na mkate mmoja tu chomboni mwao. Yesu akawaonya, akisema, "Angalieni na kujihadhari na chachu ya Mafarisayo, na pia chachu ya Herode." Wakahitimisha kuwa ni kwa sababu hawakuwa na mikate. Yesu alipotambua hayo, aliwaambia, "Mbona mnahangaika kwa sababu hamna mikate? Je, hamfahamu bado wala hamjaelewa? Je, mioyo yenu imekuwa migumu? Mna macho yasiyoona nae masikio yasiyosikia? Au hamkumbuki, nilipoimega mikate mitano na kuwapa watu elfu tano, mlijaza vikapu vingapi vya masalio?" Wakamjibu, "Saba." Akawaambia, "Bado hamjaelewa?"
Injili ya Bwana.