SOMO LA KWANZA
Yakobo 1:1—11
Mwanzo wa barua ya Mtakatifu Yakobo
Yakobo, mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, kwa makabila kumi na mawili katika mtawanyiko, salamu. Ndugu zangu, mnapopatwa na vishawishi vya namna nyingi, mvipokee kama furaha tupu. Mwajua kwamba kushawishiwa imani yenu kunaimarisha uvumilivu. Lakini uvumilivu ufuatwe na ukamilifu, muwe wakamilifu bila hitilafu katika mambo yote. Ikiwa mmoja wenu ametindikiwa hekima, ajiombee kwa Mungu atapewa, kwani Mungu apenda kuwapa wote bila kumkemea mtu. Lakini mwenye kuomba aombe kwa imani bila mashaka, kwani mwenye shaka ni kama wimbi la bahari linalotupwa na upepo huko na huko. Mtu wa namna hiyo asidhani kwamba atapata kitu kwa Bwana. Ni mtu aliyegawanyika, kigeugeu katika njia zake zote. Ndugu wa hali duni ajisifie cheo chake kikubwa, na tajiri ajisifie uduni wake, kwani atapita "kama ua la malishoni." Jua linachomoza, hari yake inaunguza malisho, ua lake linainama, na uzuri wa sura yake unatoweka. Vivyo hivyo, tajiri atafifia pamoja na matendo yake.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 119:67, 68, 71, 72, 75, 76 (K. 77a)
K. Unirehemu, ee Bwana, nipate kuishi.
Kabla ya kunyenyekeshwa, nilikuwa nimepotea,
lakini sasa nalitii neno lako. K.
Wewe ni mwema na unatenda mema;
unifundishe kanuni zako. K.
Ilikuwa vema kwangu kunyenyekeshwa,
ili nijifunze kanuni zako. K.
Sheria ya kinywa chako ina thamani kwangu zaidi
kuliko wifi wa dhahabu na fedha. K.
Najua, ee Bwana, maamuzi yako ni ya haki;
ingawa umeninyenyekeza, wewe ni mwenye haki. K.
Upendo wako uliojaa rehema unifariji
kadiri ya ahadi yako kwa mtumishi wako. K.
SHANGILIO LA INJILI
Yohane 14:6
K. Aleluya. W. Aleluya
K. Mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima, asema Bwana; hakuna ajaye kwa Baba, ila kwa njia ya yangu.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 8:11—13
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Wakati ule: Mafarisayo walifika wakaanza kujadiliana na [Yesu], wakidai ishara kutoka mbinguni ili kumjaribu, akapiga kite toka moyoni, akasema, "Mbona kizazi hiki chadai ishara? Amin, nawaambieni, kizazi hiki hakitapewa ishara." Akawaacha, akapanda tena chomboni, akavuka ng'ambo.
Injili ya Bwana