SOMO LA KWANZA
1 Wafalme 12:26—32; 13:33—34
Somo katika kitabu cha kwanza cha Wafalme
Siku zile: Yeroboamu [mfalme wa Israeli] alijisemea moyoni, "Mwisho ufalme utairudia nyumba ya Daudi. Kama watu hawa watapanda kutoa sadaka katika hekalu la Bwana Yerusalemu, mioyo yao itamwelekea Rehoboamu mfalme wa Yuda, nao wataniua mimi na kumrudia Rehoboamu mfalme wa Yuda." Baada ya kupata ushauri, mfalme akawatengeneza ndama wawili wa dhahabu na kuwaambia watu, "Mmepanda Yerusalemu kwa muda mrefu wa kutosha. Tazameni enyi Waisraeli, hii hapa miungu yenu iliyowatoa kutoka Misri." Ndama mmoja akamweka huko Betheli; na mwingine akamweka katika Dani. Jambo hili likawa sababu ya dhambi, maana watu walikwenda hadi huko Dani kuabudu. Tena akajenga vihekalu katika sehemu za juu na kuwaweka makuhani watu wasio Walawi. Yeroboamu akaweka sikukuu mwezi wa nane, siku ya kumi na tano ya mwezi kama ilivyokuwa katika Yuda, naye akapanda altareni. Akatenda jambo hili Betheli, akitolea sadaka kwa ndama wa dhahabu aliowatengeneza, ana akawaweka makuhani Betheli, hapo mahali pa juu alipopatengeneza. Yeroboamu hakuongoka na kuacha mwenendo wake mbovu, bali aliwachagua makuhani wengi zaidi wa sehemu za kuabudia za milimani kutoka miongoni mwa watu wa kawaida. Akamweka wakfu kuwa kuhani wa sehemu za kuabudia za milimani kila aliyetaka kuwa kuhani. Mwenendo huu ulikuwa dhambi kwa nyumba ya Yeroboamu, ukawa sababu ya kuangamizwa kwake na kufutwa usoni mwa nchi.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 106:6—7a, 19—20, 21—22 (K. 4a)
K. Utukumbuke, ee Bwana, kwa upendeleo ulio nao kwa taifa lako.
Tumekosa kama vile baba zetu walivyokosa.
Tumefanya uovu; tumetenda ubaya.
Baba zetu, walipokuwa Misri
hawakufahamu maana ya matendo yako makuu. K.
Huko Horebu wakafanya ndama,
wakaabudu sanamu ya chuma,
wakaubadilisha utukufu wa Mungu wao
kwa sanamu ya ng'ombe alaye majani. K.
Wakamsahau Mungu mwokozi wao,
aliyefanya makuu huko Misri,
na miujiza katika nchi ya Hamu,
mambo ya kutisha katika Bahari ya Shamu. K.
SHANGILIO LA INJILI
Mathayo 4:4b
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo kinywani mwa Mungu.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 8:1—10
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Siku zile, pale umati mkubwa wa watu ulipokusanyika, nao walikosa chakula, Yesu aliwaita wafuasi wake, akawaambia, "Nauhurumia umati huu wa watu kwa maana siku tatu wameshinda nami. Sasa hawana chakula. Nikiwaaga waende nyumbani kwa njaa, watazimia njiani, maana baadhi yao wametoka mbali." Wafuasi wake wakamjibu, "Itawezekanaje kuwashibisha mikate hapa nyikani?" Akawauliza, "Mna mikate mingapi?" Wakasema, "Saba." Akawaamuru watu wakae chini. Akaitwaa ile mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wafuasi wake waigawe, nao wakawagawia watu. Kadhalika walikuwa na samaki wachache. Akawabariki, akaamuru wagawiwe pia. Wakala, wakashiba. Wakakusanya mabaki yaliyosalia, jumla makapu saba. Nao waliokula walikuwa elfu nne. Akawaaga na akapanda chomboni pamoja na wafuasi wake, akafika eneo la Dalmanutha.
Injili ya Bwana.