SOMO LA KWANZA
1 Wafalme 11:29—32; 12:19
Somo katika kitabu cha kwanza cha Wafalme
Wakati ule: Yeroboamu aliondoka Yerusalemu akakukatana njiani na nabii Ahiya, Mshiloni. Ahiya alikuwa amevaa kanzu mpya, na hao wawili walipokuwa peke yao shambani, Ahiya alivua ile kanzu yake mpya na kuichana vipande kumi na viwili. Akamwambia Yeroboamu, "Twaa wewe vipande kumi, maana Bwana Mungu wa Israeli asema hivi: Tazama nitaurarua ufalme, na kuuondoa katika mkono wa Sulemani, na kukupa wewe makabila kumi. Naye nitamwachia kabila moja kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu na kwa ajili ya Yerusalemu, mji niliojichagulia miongoni mwa makabila yote ya Israeli." Hivyo ndivyo Waisraeli walivyoiasi nyumba ya Daudi, hata leo.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 81:10—11ab, 12—13, 14—15
K. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu: isikieni sauti yangu.
Asiwepo kwako mungu wa kigeni,
wala usimwabudu mungu mwingine.
Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,
niliyekupandisha kutoka nchi ya Misri. K.
Lakini taifa langu halikuisikia sauti yangu,
wala Israeli hakunitii.
Basi, nikawaacha wafuate ugumu wa mioyo yao,
waende kwa kadiri ya mipango yao. K.
Laiti watu wangu wangenisikiliza,
kama Israeli angeenenda katika njia zangu!
Mara ningewagandamiza adui zao,
ningeugeuza mkono wangu dhidi ya watesi wao. K.
SHANGILIO LA INJILI
Matendo Ya Mitume 16:14b
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Utufungue mioyo yetu, ee Bwana, tupate kuyasikia maneno ya Mwanao.
Aleluya.
INJILI
Marko 7:31—37
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko.
Wakati ule: Yesu alirudi kutoka wilaya ya Tiro, kwa njia ya Sidoni, akipita katikati ya Dekapoli, akafikia ziwa la Galilaya. Wakamletea bubu-kiziwi, wakamwomba amwekee mkono. Akamtenga na umati wa watu, akamtia vidole masikioni, akatema mate na kumgusa ulimi; akatazama juu mbinguni, akapiga kite, akamwambia, "Effathà!" (maana yake, 'Fumbuka!'). Mara akafumbuka masikio na akafunguliwa kifungo cha ulimi wake, akaongea sawasawa. Akawakataza wasimwambie mtu. Lakini kadiri alivyowakataza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari zake. Walishangaa kupita kiasi, wakasema, "Amefanya yote vema, awajalia viziwi wasikie, na bubu waongee."
Injili ya Bwana.