SOMO LA KWANZA
1 Wafalme 11:4—13
Somo katika kitabu cha kwanza cha Wafalme
Sulemani alipokuwa mzee, wake zake waliugeuza moyo wake, akaifuata miungu ya kigeni, na wala moyo wake haukuwa upande wa Bwana, kama moyo wa Daudi baba yake ulivyokuwa. Sulemani alimfuata Astarte, mungu-mke wa Wasidoni na Milkomu aliye chukizo la Waamoni. Sulemani alifanya mabaya machoni pa Bwana, wala hakumfuata Bwana kikamilifu kama Daudi baba yake. Sulemani akamjengea Kemoshi, chukizo la Wamoabu, sehemu za kuabudia za milimani, katika mlima mkabala na Yerusalemu, na kwa Moleki aliye chukizo la Waamoni. Akawafanyia wake wote wa kigeni vivyo hivyo ili wapate kuifukizia miungu yao ubani na kuitolea sadaka. Kwa hiyo Bwana akamkasirikia Sulemani kwa kuwa moyo wake umegeuka na kumwacha Bwana, Mungu wa Israeli, aliyemtokea mara mbili na akamkanya wazi kutokuiabudu miungu ya kigeni, lakini Sulemani hakuyatii maagizo ya Bwana. Basi Bwana akamwambia Sulemani: Kwa kuwa umeyafanya hayo, bila kuyashika maagano yangu, na amri zangu nilizokupa, nitaurarua ufalme kutoka kwako na kumpa mtumishi wako. Lakini sitafanya hivyo wakati wa maisha yako, kwa ajili ya Daudi baba yako, nitaugawa katika mkono wa mwanao. Wala sitamnyang'anya ufalme wote, bali nitampa mwanao kabila moja kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, na kwa ajili ya Yerusalemu nilioichagua.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 106:3—4, 35—36, 37 na 40 (K. 4a)
K. Utukumbuke, ee Bwana, kwa upendeleo ulio nao kwa watu wako.
Heri wenye kushika yaliyo haki,
na kutenda yaliyo kweli wakati wote.
Unikumbuke kwa, ee Bwana,
kwa upendeleo ulio nao kwa taifa lako.
Nitembelee ukiwa na wokovu wako, K.
Lakini walichanganyika na mataifa,
wakajifunza desturi zao.
Wakazitumikia sanamu zao,
nazo zikawa mtego uliowatega. K.
Waliwatolea wana wao na binti zao,
kuwa sadaka kwa mashetani.
Hasira ya Bwana ikawaka juu ya watu wake;
akawachukia watu wa urithi wake. K.
SHANGILIO LA INJILI
Yakobo 1:21bc
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Lipokeeni kwa upole neno lililopandwa ndani mwenu, ndilo neno liwezalo kuziokoa roho zenu.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 7:24—30
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Wakati ule: Yesu aliondoka, akaenda pande za Tiro na Sidoni. Huko aliingia katika nyumba moja kwa kujificha asijulikane, lakini hakuweza kujificha. Mara mwanamke mmoja alipata habari. Binti yake alikuwa amepagawa na pepo mchafu. Akaja, akamwangukia miguuni pake. Mwanamke huyo alikuwa mpagani Msirofoinike. Akamwomba amfukuze pepo mbaya katika binti yake. Alimwambia, "Kwanza watoto washibe, kwa maana si sawa kuwanyima watoto chakula na kuwatupia vijibwa." Naye akamjibu, " Bwana, lakini hata vijibwa vilivyo chini ya meza hula mabaki ya watoto yanayodondoka." Yesu akamwambia, "Kwa sababu ya neno hilo, uende. Pepo mbaya amemtoka binti yako." Alipoenda nyumbani kwake, akamkuta msichana amelala kitandani, na pepo mbaya amekwisha kumwacha.
Injili ya Bwana.