SOMO LA KWANZA
1 Wafalme 10:1—10
Somo katika kitabu cha kwanza cha Wafalme
Siku zile: Malkia wa Sheba aliposikia umaarufu wa Sulemani alimjia ili kumjaribu kwa maswali ya mafumbo. Alifika Yerusalemu na wafuasi wengi sana na ngamia waliochukua manukato, dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani. Alipofika kwa Sulemani alimwuliza yote aliyokuwa nayo moyoni mwake. Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote, wala hakukuwa na neno aliloshindwa kumfumbulia. Basi malkia wa Sheba alipoona hekima nyingi za Sulemani, na nyumba aliyoijenga, na chakula kilichowekwa mezani pake, na watumishi walivyokaa, na wahudumu wake walivyosimama na mavazi yao, na wanyweshaji wake, na sadaka alizotolea hekaluni mwa Bwana, aliishiwa pumzi. "Habari nilizosikia nchini mwangu juu ya matendo yako na hekima zako ni za kweli," alimwambia mfalme. "Ingawa sikusadiki habari hizo, mpaka nimefika na kuona yote kwa macho yangu, nimegundua kuwa hata nusu sikuambiwa. Kwa maana hekima yako imezidi, na kufanikiwa sana kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, heri hawa watumishi wako, wanaosimama mbele yako daima, wakisikia hekima yako. Na ahimidiwe Bwana Mungu wako, aliyependezwa nawe na kukuweka juu ya kiti cha ufalme wa Israeli. Kwa upendo wake wa milele kwa Israeli, Bwana amekufanya mfalme juu yake ili utende hukumu na haki." Kisha akampa mfalme talanta mia moja na ishirini za dhahabu, na manukato mengi sana, na vito vya thamani. Wala hakutokea tena mtu aliyemletea mfalme Sulemani uwingi wa manukato kama malkia wa Sheba.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 37:5—6, 30—31, 39—40 (K. 30a)
K. Kinywa cha mwenye haki hunena hekima.
Umkabithi Bwana njia yako;
mtumainie naye atatenda,
na ufanye unyofu wako ung'are kama mwanga,
na haki ya njia yako kama jua la adhuhuri. K.
Kinywa cha mtu mwenye haki hunena hekima,
ulimi wake husema yaliyo kweli.
Sheria ya Mungu imo moyoni mwake;
hatua zake hazitateleza. K.
Wokovu wa wenye haki watoka kwa Bwana,
yeye ni kimbilio lao wakati wa shida.
Bwana huwasaidia na kuwaopoa,
huwaopoa na waovu, na kuwakomboa:
kwa kuwa wamemkimbilia Mungu. K.
SHANGILIO LA INJILI
TAZAMA YOHANE 17:17b, a
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Neno lako, ee Bwana, ni kweli; ututakase kwa hiyo kweli.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 7:14–23
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Wakati ule: Yesu aliwaita watu tena, akawaambia, "Nisikieni, ninyi nyote, na eleweni. Hakuna kitu kinachomwingia mtu kutoka nje kinachoweza kumnajisi; bali vitu vimtokavyo mtu vyamtia unajisi." Alipowaacha watu na kuingia nyumbani, wafuasi wake walimwuliza maana ya mfano. Naye akawaambia, "Yaani, hata ninyi hamna ufahamu? Hamwelewi ya kuwa kitu kinachomwingia mtu kutoka nje hakiwezi kumnajisi, kwa maana hakimwingii moyoni, ila tumboni? Kutoka humo chaondoshwa kikaishia chooni." (Kwa kusema hivi alitangaza ya kuwa vyakula vyote ni halali.) "Lakini yamtokayo mtu ndiyo yanayomnajisi. Kwa maana kutoka ndani ya mtu, kutoka mioyoni mwao, yanatoka mawazo mabaya: uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, choyo, ukorofi, hila, ufisadi, wivu, matusi, kiburi, upumbavu. Maovu hayo yote yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi."
Injili ya Bwana.