SOMO LA KWANZA
1 Wafalme 8:1—7, 9—13
Somo katika kitabu cha kwanza cha Wafalme
Siku zile: Sulemani aliwakusanya wazee wa Israeli, na wakuu wote wa kabila na wakuu wa koo za mababa wa Israeli, wakakusanya na kumwendea mfalme Sulemani huko Yerusalemu, ili kulipandisha sanduku la agano la Bwana kutoka mji wa Daudi (yaani Sioni). Watu wote wa Israeli wakakutana mbele ya mfalme Sulemani wakati wa sikukuu, katika mwezi wa Ethanimu (ndio mwezi wa saba). Wazee wote wa Israeli walipofika, makuhani wakalichukua sanduku la agano; wakalipeleka juu ya sanduku la Bwana pamoja na hema ya kukutania, na vyombo vyote vitakatifu vilivyokuwepo. Makuhani na Walawi walivibeba. Mfalme Sulemani mwenyewe alikuwako, na Waisraeli wote waliokutanika kwa ajili ya tukio hilo, walitolea sadaka za ng'ombe na kondoo wengi sana wasio na idadi. Makuhani wakalipeleka sanduku la agano mahali pake, ndani ya hekalu, Patakatifu pa Patakatifu, na wakaliweka chini ya mbawa za makeburi. Hayo makerubi yakanyosha mbawa zao juu ya sanduku na kulifunika pamoja na miti yake. Mle ndani mwa sanduku hakukuwa na kitu isipokuwa zile mbao mbili za mawe ambazo Musa aliweka ndani huko Horebu, Bwana alipofanya agano na Waisraeli, walipotoka katika nchi ya Misri. Mara makuhani walipotoka katika Patakatifu, wingu likaijaza nyumba ya Bwana, hata makuhani hawakuweza kufanya kazi yao ya utumishi kwa maana utukufu wa Bwana ulilijaza hekalu lake. Ndipo Sulemani akanena, "Bwana amekusudia kukaa katika wingu nene, nami nimekujengea kweli nyumba ya kukaa, mahali pa makao yako milele."
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 132:6—7, 8—10 (K. 8a)
K. Inuka, ee Bwana, uende mahali pako pa kupumzika.
Tazama, tulisikia habari zake katika Efratha;
tulilikuta katika mashamba ya Yaari.
Na tuingie katika maskani yake;
tusujudu penye kibao cha kuwekea miguu yake. K.
Inuka, ee Bwana, uende mahali pa pumziko lako,
wewe na sanduku la nguvu zako.
Makuhani wako na wavikwe haki;
na watakatifu wako washangilie kwa furaha.
Kwa ajili ya Daudi, mtumishi wako,
usimkatae mpakwa wako. K.
SHANGILIO LA INJILI
Mathayo 4:23
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Yesu alitangaza Injili ya ufalme na kuponya magonjwa yao yote.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 6:53—56
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Wakati ule: [Yesu na wafuasi wake] walielekea pwani, wakafika Genesareti na wakatia nanga. Walipotoka chomboni, watu walimtambua. Kwa haraka wakaizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwapeleka wagonjwa katika machela kila mahali waliposikia yupo. Basi kila alikoenda, iwe vijijini, mijini au kiungani, waliwaweka wagonjwa uwanjani, wakamsihi awaruhusu waguse walau pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa walipona.
Injili ya Bwana.