SOMO LA KWANZA
Ayubu 7:1—4, 6—7
Somo katika kitabu cha Ayubu
Ayubu alisema: Je, mtu Hana kazi ngumu duniani? Hatumiki kama mtu wa mshahara? Kama mtumwa anayetamani kivuli kidogo; kama mfanyakazi anayetazamia mshahara wake, ndivyo nami napata miezi ya usumbufu na kupewa siku za mateso. Nilalapo kitandani najiisemea: kutakucha wakati gani? Nikiamka naona kwamba jioni inakawia! Hivi nazidi kusumbuka nahangaika hadi mapambazuko. Siku zangu hupita upesi kama chombo cha mfumaji; hupita bila matumaini. Kumbuka ya kwamba uzima wangu ni pumzi tu; macho yangu hayataona furaha tena.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 147:1—2, 3—4, 5—6 (K. tazama 3a)
K. Msifuni Bwana, yeye anawaponya waliovunjika moyo.
Jinsi gani ni vema kumwimbia Mungu wetu sifa;
kwa maana kwapendeza, na yastahili kumsifu yeye.
Bwana anaijenga Yerusalemu,
anawakusanya Waisraeli waliotawanyika. K.
Yeye anawaponya waliovunjika moyo,
na kuvitibu vidonda vyao,
ameiweka idadi ya nyota,
anaziita zote kwa jina. K.
Bwana wetu ni mkuu na mwenye nguvu nyingi,
hekima yake haina kikomo.
Bwana huwategemeza wanyonge,
huwaangusha waovu mpaka chini. K.
SOMO LA PILI
1 Wakorintho 9:16—19, 22—23
Somo kutoka Barua ya kwanza ya Paulo kwa Wakorintho.
Ndugu zangu: Nikiihubiri Injili, sina sababu ya kujisifu. Wajibu huo nimetwikwa. Ole wangu nisipoihubiri Injili. Maana nikifanya kazi hii kwa hiari, nitatuzwa. Lakini nisipoichagua mwenyewe, nimekabidhiwa madaraka tu. Hapo tuzo yangu ni nini? Ni hili: nihubiri Injili bila kudai kitu, wala kutumia haki yangu ninayopewa na Injili. Maana hivyo nina uhuru kwa wote, naweza kujifanya mtumishi wa watu wote, nipate kuwavuta wengi zaidi. Kwa watu dhaifu nalikuwa dhaifu, nipate kuwavuta wadhaifu. Nimekuwa yote kwa wote, nipate kuwaokoa walau baadhi yao kwa namna yotote. Hayo yote nayafanya kwa ajili ya Injili, nipate kuwa mshiriki wake.
Neno la Bwana.
SHANGILIO LA INJILI
Mathayo 8:17
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Kristo mwenyewe amejitwika udhaifu wetu, amechukua magonjwa yetu.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 1:29—39
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Wakati ule: Yesu alipotoka kwenye sinagogi, alikwenda mara pamoja na Yakobo na Yohane katika nyumba ya Simoni na Andrea. Hapo mkwewe Simoni alikuwa amelala kitandani akishikwa na homa. Mara wakampasha habari ya hali yake. Akamkaribia, akamshika mkono na kumwinua. Mara moja homa ikamwacha na akawatumikia. Ilipofika jioni, baada kuzama jua, walimletea wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wabaya. Mji mzima walikusanyika mlangoni pake. Akawaponya wengi waliokuwa na magonjwa mbalimbali. Akatoa pepo wabaya wengi, wala hakuwaruhusu kusema, kwa kuwa walimjua. Asubuhi na mapema, kabla ya kupambazuka, aliamka, akaondoka, na kwenda mahali pa nyika ili kusali. Simoni na wenziwe wakamtafuta na walipomwona, wakasema, "Watu wote wanakutafuta." Akawaambia, "Twendeni mahali pengine katika vijiji vya jirani, nipate kuhubiri huko pia. Hiyo ndiyo nia ya kuja kwangu." Basi alitembea nchi yote ya Galilaya alihubiri katika masinagogi yao na kuwatoa pepo wabaya.
Injili ya Bwana.