RANGI YA KILITURJIA: ZAMBARAU 💜
SOMO LA KWANZA
KUTOKA 20:1—17
Amri inatolewa kupitia Musa.
Somo katika kitabu cha Kutoka
Siku zile: Mungu alisema maneno haya yote: Ndimi Bwana Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya watumwa. Usiwe na miungu mingine ila yangu. Usijifanyizie sanamu ya kuchonga wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usizisujudie sanamu hizo wala usizitumikie, kwa maana mimi, Bwana Mungu wako, mimi ni Mungu mwenye wivu, ninayeyapatiliza maovu ya baba juu ya watoto, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, lakini nawafanyia rehema vizazi maelfu vya wale wanipendao na kuzishika amri zangu. Usilitaje bure jina la Bwana Mungu wako, kwa maana Bwana hataacha kumwadhibu mwenye kulitaja jina lake bure. Ikumbuke siku ya Sabato, uitakase. Siku sita fanya kazi, ufanye kazi zako zote, lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako. Siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumishi wako, wala mjakazi wako, wala wanyama wako wa kazi, wala mgeni anayekaa kwako. Maana kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, nchi, bahari na vyote vilivyomo, lakini alipumzika siku ya saba. Ndiyo maana Bwana ameibariki siku ya Sabato na kuifanya takatifu. Waheshimu baba yako na mama yako, upate kuwa na maisha marefu katika nchi upewayo na Bwana Mungu wako. Usiue. Usizini. Usiibe. Usimshuhudie jirani yako uongo. Usiitamani nyumba ya jirani yako. Usimtamani mke wa jirani yako, wala mtumishi wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala kitu chochote kilicho mali ya jirani yako."
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 19:8, 9, 10, 11 (K. tazama Yohane 6:68c)
K. Bwana, wewe una maneno ya uzima wa milele.
Sheria ya Bwana ni kamilifu; yatuliza roho.
Maagizo ya Bwana ni imara;
yamletea mjinga hekima. K.
Amri za Bwana ni za haki, zaufurahisha moyo.
Agizo la Bwana ni safi,
layatia macho mwangaza. K.
Uchaji wa Bwana ni safi, hudumu hata milele.
Hukumu za Bwana ni kweli, zote ni za haki kamili. K.
Zatamanika kuliko dhahabu, kuliko wingi wa dhahabu safi.
Ni tamu kuliko asali, kuliko sega la asali. K.
SOMO LA PILI
1 WAKORINTHO 1:22—25
Sisi tunamhubiri Kristo msulubiwa, aliye kikwazo kwa binadamu, lakini kwa waliotwa, hekima ya Mungu.
Somo katika barua ya kwanza ya Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho
Ndugu zangu: Wayahudi hudai ishara, Wagiriki hutafuta hekima, bali sisi tunamhubiri Kristo msulibiwa, aliye kikwazo kwa Wayahudi na ujinga kwa watu wa mataifa. Lakini kwa walioitwa, Wayahudi kwa Wagiriki, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu. Kwa maana ujinga wa Mungu una hekima ipitayo hekima ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi kuliko nguvu za wanadamu.
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
INJILI
YOHANE 2:13—22
Yeye alizungumzia hekalu la mwili wake.
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Yohane
Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia. Yesu alipanda kwenda Yerusalemu. Akaona pale hekaluni watu wakiuza ng'ombe, kondoo, na njiwa, pia wabadilisha fedha wamekaa mezani pao. Akafanya mjeledi kwa kamba, akawafukuza wote katika hekalu pamoja na kondoo na ng'ombe. Akamwaga fedha za wabadilisha fedha, akapindua meza zao, akawaambia wauza njiwa, "Ondoeni vitu hivi, msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara." Wafuasi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, "Wivu wa nyumba yako unaniua." Hapo Wayahudi wakamrudia na kumwambia, "Je, utaweza kutuonyesha ishara gani inayokuruhusu kufanya hayo?" Yesu akajibu, akawaambia, "Livunjeni hekalu hili, nami nitalijenga tena kwa siku tatu." Wayahudi wakamwambia, "Miaka arobaini na sita ilitakiwa kujenga hekalu hili, na wewe utalijenga kwa siku tatu?" Lakini yeye alikuwa anazungumzia hekalu la mwili wake. Baada ya ufufuko wake katika wafu, wafuasi wake wakakumbuka ya kuwa alisema hayo, n wakayasadiki Maandiko na maneno aliyokuwa ameyasema Yesu. Alipokuwa Yerusalemu kwa sikukuu ya pasaka, watu wengi walisadiki jina lake walipoziona ishara alizozifanya. Lakini Yesu mwenyewe hakuwa na imani nao, kwa maana aliwafahamu wote, wala hakuhitaji ushuhuda wa mtu yeyote, kwa maana aliyajua yaliyomo ndani ya mtu.
INJILI YA BWANA... SIFA KWAKO EE KRISTO