SOMO 1
1 Yohane 2:3—11
Wapendwa: Hakika ya kuwa tumemjua Yesu Kristo twaipata tukizishika amri zake. Kila asemaye, "Nimemjua," lakini hashiki amri hii zake, ni mwongo, na ukweli haumo ndani yake. Lakini ashikaye neno lake, huyo bila shaka amekamilika katika upendo wa Mungu. Kwa hali hiyo twajua ya kuwa tumo ndani yake. Asemaye ya kuwa yumo ndani yake daima, sharti ayapange maisha yake kama yeye alivyoyapanga. Wapendwa, siwaandikieni amri mpya, ila amri ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Hiyo amri ya zamani ni neno mlilolisikia. Aidha ni amri mpya ninayowaandikieni, nayo ni kweli, imedhihirika ndani yake na ndani yenu; giza linatoweka, na mwanga wa kweli umeanza kung'aa. Asemaye yumo mwangani, lakini anamchukia ndugu yake, yumo bado gizani mpaka sasa. Ampendaye ndugu yake anaishi mwangani, ni kikwazo hakimo ndani yake. Amchukiaye ndugu yake yumo gizani, anatembea gizani, na hajui aendako, kwa maana giza limempofusha macho.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 96:1—2a, 2b—3, 5b—6 (K. 11a)
K. Mbinguni na zifurahi, nchi na ishangilie.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
mwimbieni Bwana, nchi yote.
Mwimbieni Bwana, lisifuni jina lake. K.
Siku kwa siku tangazeni wokovu wake.
Uhubirini utukufu wake katika mataifa;
maajabu yake, kati ya watu wote. K.
Lakini Bwana amezifanya mbingu.
Fahari na adhama zinamtangulia;
nguvu na utukufu zimo katika patakatifu pake. K.
SHANGILIO LA INJILI
LUKA 2:32
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mwanga wa kuwaangazia mataifa, na utukufu wa taifa lako Israeli.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 2:22—35
Zilipotimia siku zao za kutakasika zilizoamriwa katika Sheria ya Musa, [Maria na Yosefu] walimpeleka Yerusalemu ili wamtoe kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, "Kila mtoto wa kiume aliye mzaliwa wa kwanza awekwe wakfu kwa Bwana,") na watoe sadaka kama ilivyotajwa katika sheria ya Bwana, "hua wawili au makinda mawili ya njiwa." Huko Yerusalemu palikuwa na mtu jina lake Simeoni. Alikuwa mtu mwadilifu, mcha Mungu, naye alitazamia faraja ya Israeli na Roho Mtakatifu alikuwa naye. Alikuwa amejulishwa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Akaongozwa na Roho aende hekaluni; wakati wazazi walipomleta mtoto Yesu humo, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, akampokea mtoto mikononi mwake, akamtukuza Mungu akisema: "Sasa, ee Bwana, waweza kumruhusu mtumishi wako aende kwa amani kama ulivyonena, maana macho yangu yameuona wokovu wako, ulioandaa mbele ya watu wote, mwanga wa kuwaangazia Mataifa, na utukufu wa taifa lako Israeli." Baba na mama yake walishangazwa na maneno yaliyosemwa juu yake; Simeoni akawabariki, na akamwambia Maria mama yake, "Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi katika Israeli, tena kama alama itakayokataliwa, na upanga utakupenya moyoni, ili mawazo ya mioyo mingi yafunuliwe."
Injili ya Bwana.