SOMO 1
Matendo Ya Mitume 6:8—10, 12; 7:54—60
Siku zile: Stefano, aliyejaa neema na nguvu, alifanya miujiza na ishara kubwa kati ya watu. Lakini baadhi ya washiriki wa sinagogi lililoitwa Sinagogi la Walio Huru, na la Wakirene na la Waleksandria, hata watu wa Silisia na Asia, walisimama wabishane na Stefano, lakini hawakuweza kuishinda hekima na Roho aliyesema ndani yake. Wakawachochea watu, na wazee, na Waandishi, wakamngojea, wakamkamata na kumpeleka barazani. [Wote waliohudhuria barazani,] waliposikia maneno yake, walighadhabika moyoni, wakamkerezea meno. Lakini Stefano, aliyejaa Roho Mtakatifu, alielekeza macho mbinguni, akaona utukufu wa Mungu na Yesu amesimama kuume kwa Mungu, akawaambia, "Tazameni, ninaziona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Mtu amesimama kuume kwa Mungu." Nao wakapiga makelele sana, wakajiziba masikio, wakamshambulia kwa nia moja. Wakamburuza nje ya mji, wakampiga mawe. Mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja, jina lake Sauli. Basi, walipokuwa wakimtupia mawe Stefano, yeye alisali na kuita, "Bwana Yesu, ipokee roho yangu." Akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa, "Bwana, usiwahesabie dhambi hii." Baada ya maneno hayo alikata roho.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 31:3bc—4, 6 na 8ab, 16bc na 17
K. Mikononi mwako, ee Bwana, naiweka roho yangu.
Uwe kwangu mwamba wa kukimbilia,
ngome imara ya kuniokoa.
Kwa maana wewe u mwamba wangu na ngome yangu;
kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge. K.
Mikononi mwako naiweka roho yangu;
uniokoe, ee Bwana, Mungu wa kweli.
Nitaushangilia n kuufurahia wema wako,
kwa kuwa umeangalia umaskini wangu. K.
Uniponye na mikono ya adui zangu
na wadhulumu wangu.
Umwangazie mtumishi wako uso wako;
unisalimishe kwa wema wako. K.
SHANGILIO LA INJILI
ZABURI 118:26ab, 27a
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mbarikiwa yeye ajaye kwa jina la Bwana. Bwana ni Mungu, naye ametuangazia.
W. Aleluya.
INJILI
Mathayo 10:17—22
Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake, "Jihadharini na watu, kwa maana watawapeleka barazani, na watawapiga katika masinagogi. Mtachukuliwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili mtoe ushuhuda kwao na kwa watu wa mataifa. Basi, wanapowapeleka barazani, msihangaike juu ya nini cha kusema na namna gani, kwa maana saa ile mtapewa la kusema. Kwani si ninyi msemao, bali Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. Ndugu atamtoa ndugu auawe, kadhalika baba atamtoa mwana. Na watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua. Na mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu. Lakini mtu aliye thabiti mpaka mwisho atasalimika."
Injili ya Bwana.