SOMO 1
Isaya 40:1—11
Watulizeni, wapeni tulizo watu wangu, asema Mungu wenu. Semeni na moyo wa Yerusalemu, utangazieni ya kwamba: Huduma yake ngumu imekwisha, dhambi yake imeondolewa, maana kwa mkono wa Bwana amepokea adhabu maradufu kwa maovu yake yote. Mtu analia: tengenezeni jangwani njia ya Bwana! Nyosheni nyikani barabara kwa Mungu wetu! Kila bonde lifukiwe, kila na kilima kishushwe, njia zenye kupotoka zinyoshwe, na njia zenye mashimo zisawazishwe. Hapo utukufu wa Bwana utafunuliwa, na watu wote watauona mara; maana kinywa cha Bwana kimenena haya. Kuna sauti isemayo, "Tangazeni." Nikajibu, "Nitangaze nini?" "Wote wenye mwili ni kama nyasi, na wema wake wote ni kama ua la shambani. Majani hunyauka na maua husinyaa, kwa sababu pumzi ya Bwana yavuma juu yake." "Hakika binadamu ni majani! Majani hunyauka na maua husinyaa, lakini neno la Mungu wetu litasimama milele." Panda juu ya mlima mrefu, uitangaziye Sioni habari njema! Paza sauti kwa nguvu, uitangaziye Yerusalemu habari njema! Paza sauti, usiogope! Sema kwa miji ya Yuda: Tazama, Mungu wenu! Yupo hapa Bwana Mungu: anakuja kwa uwezo, na mkono wake utatawala; tuzo ya ushindi wake litamsindikiza, mateka yake yatamtangulia. Kama mchungaji, anachunga kundi lake; mkononi mwake atawakusanya wanakondoo, atawachukua kifuani mwake, atawaongoza kondoo wenye kunyonyesha.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 96:1—2, 3, na 10ac, 11—12, 13
K. Bwana Mungu wetu anakuja kwa uwezo.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya;
mwimbieni Bwana, nchi yote.
Mwimbieni Bwana, lisifuni jina lake;
siku kwa siku tangazeni wokovu wake. K.
Uhubirini utukufu wake kati ya mataifa;
maajabu yake, kati ya watu wote.
Waambieni mataifa: Bwana ni Mfalme.
atawahukumu watu kwa haki. K.
Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie;
bahari na ivume na vyote viijazavyo;
mashamba na yachangamke, na vyote vilivyomo.
Ndipo miti yote ya msituni iimbe kwa furaha. K.
Mbele za Bwana, kwa kuwa anakuja.
Kwa kuwa anakuja kuihukumu nchi;
atahukumu ulimwengu kwa haki,
nayo mataifa kwa uaminifu wake. K.
SHANGILIO LA INJILI
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Siku ya Bwana iko karibu; tazama, atakuja kutuokoa.
W. Aleluya.
INJILI
Mathayo 18:12—14
Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake: "Mwaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, akapotewa na mmoja wao, je, hawaachi wale tisini na tisa milimani, akaenda kumtafuta yule aliyepotea? Na baada ya kumwona, amin, nawaambieni, anafurahi zaidi juu ya huyo kuliko juu ya wale tisini na tisa wasiopotea. Vivyo hivyo haimpendezi Baba yenu wa mbinguni, mmoja wa wadogo hawa apotee."
Injili ya Bwana.