SOMO 1
Isaya 35:1—10
Jangwa na pori vitafurahi; nyika ishangilie na kuchanua majani; itoe maua mengi kama yasmini, iimbe, na ishangilie kwa furaha. Imepewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na wa Sharoni; utukufu wa Bwana utaonekana, ukuu wa Mungu wetu. Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, fanyeni imara magoti yaliyolegea. Wale waliovunjika moyo, waambieni: mjipe moyo, msiogope! "Tazameni, Mungu wetu yupo hapa atalipiza kisasi; adhabu itakuja kutoka kwa Mungu, naye atakuja kuwaokoa ninyi." Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, masikio ya viziwi yatafunguliwa; ndipo kiwete atarukaruka kama swala, na ulimi wa bubu utaimba kwa furaha. Maji yatabubujika katika jangwa, na vijito katika nyika. Nchi kavu itageuka kuwa ziwa la maji, na nchi ya kiu itakuwa chemchemi za maji. Makao walipolala mbweha yatageuka kuwa vichaka vya matete na nyasi. Patakuwapo na barabara kuu, nayo itaitwa njia takatifu; wasio safi hawataruhusiwa pale, bali itakuwa kwa ajili ya watu wake, msafiri wala mpumbavu hawatapotea katika njia hiyo. Hapo hapatakuwa na simba, wala mnyama mkali hatapita huko, wala hatapatikana pale. Lakini waliokombolewa ndio watakaotembea katika njia hiyo. Nao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sioni wakishangilia. Furaha ya milele itapamba vichwa vyao; nao watafanya sherehe na shangwe, huzuni na kilio vitakimbia.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 85:9ab—10, 11—12, 13—14
K. Mungu wetu atakuja na kutuokoa!
Ninasikia anayosema Bwana Mungu;
hakika, anasema maneno ya amani
na watu wake na waamini wake.
Wokovu wake ni karibu nao wenye kumcha;
utukufu wake utakaa katika nchi yetu. K.
Wema na uaminifu zitakutana;
haki na amani zitabusiana.
Uaminifu utachipuka katika nchi;
na haki itachungulia kutoka mbinguni. K.
Naye Bwana atatoa yaliyo mema;
na nchi yetu itatoa mazao.
Haki itatangulia mbele ya Bwana,
wokovu utafuata nyayo zake. K.
SHANGILIO LA INJILI
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Tazama, Mfalme anakuja, Bwana wa mbingu na nchi, na ataivunja nira ya utumwa wetu.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 5:17—26
Siku moja Yesu alipokuwa akifundisha, Mafarisayo na Walimu wa sheria walikuwa wamekuja toka kila kijiji cha Galilaya na Yudea na Yerusalemu, wakakaa pale, na nguvu ya Bwana ya kuponya ilikuwa naye. Hapo watu wakamletea mwenye kupooza, wakajaribu kumpeleka ndani na kumweka mbele yake. Lakini walipokosa nafasi ya kumpeleka ndani kwa sababu ya msongamano wa watu, walipanda juu kwenye paa, wakaondoa vigae, wakamteremsha pamoja na kitanda chake, wakamweka mbele ya Yesu. Naye alipoona imani yao, alimwambia, "Mwanangu, umeondolewa dhambi zako." Mara hapo Waandishi na Mafarisayo wakaanza kuwaza moyoni na kujiambia, "Nani huyu asemaye maneno ya kukufuru? Nani aweza kuondolea dhambi ila Mungu peke yake?" Yesu, lakini, alijua mawazo yao akajibu akawaambia, "Mnawaza nini mioyoni mwenu? Je, ni lipi rahisi zaidi, kusema, 'Umeondolewa dhambi zako,' au kusema, 'Simama, uende?' Lakini mpate kujua ya kuwa Mwana wa Mtu anao uwezo wa kuondolea dhambi duniani," — akamwambia mwenye kupooza, — "Nakuambia, simama, jitwike kitanda chako, nenda nyumbani kwako." Mara akasimama mbele yao, akajitwika kitanda, akaenda nyumbani kwake akimtukuza Mungu. Mshangao ukawashika wote, nao wakamtukuza Mungu, wakajaa uchaji wakisema, "Leo tumeona maajabu."
Injili ya Bwana.