SOMO 1
Isaya 25:6—10a
Katika mlima huu, Bwana wa majeshi atawaandalia mataifa yote karamu ya nyama nono, karamu ya divai iliyo bora, karamu ya nyama yenye mafuta, ya divai iliyotakata kabisa. Juu ya mlima huu ataharibu kifuniko kilicho juu ya makabila yote; na kitambaa kilichotandwa juu ya mataifa yote. Ataharibu mauti hata milele. Bwana Mungu atapangusa machozi katika nyuso zote; ataondoa aibu ya taifa lake katika dunia yote, maana Bwana amesema hivyo. Katika siku hiyo watasema, "Tazameni, huyu ndiye Mungu wetu; tulimtumainia ili atuokoe, ndiye Bwana tuliyemtumainia; tushangilie na kuufurahia ukombozi wake!" Maana mkono wa Bwana utatua juu ya mlima huu.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 23:1—3a, 3b—4, 5, 6 (K. 6cd)
K. Nitakaa nyumbani mwa Bwana kwa miaka mingi ijayo.
Bwana ndiye mchungaji wangu,
sitapungukiwa na kitu.
Hunipumzisha katika malisho mabichi;
hunipeleka kwenye maji matulivu; hunipatia nguvu. K.
Huniongoza katika njia zilizo sawa / kwa ajili ya jina lake.
Hata nijapopita katika bonde la giza,
siogopi mabaya, kwani wewe upo pamoja nami;
gongo lako na fimbo yako vyanituliza. K.
Waandaa meza mbele yangu,
machoni pa adui zangu;
umenipaka mafuta kichwani;
kikombe changu kinafurika. K.
Kweli, wema na fadhili zitanifuata
siku zote za maisha yangu.
Nitakaa nyumbani mwa Bwana
kwa miaka mingi ijayo. K.
SHANGILIO LA INJILI
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Tazama, Bwana anakuja kuwakomboa watu wake; wana heri waliotayari kumlaki.
W. Aleluya.
INJILI
Mathayo 15:29—37
Wakati ule: Yesu alifika kando ya Bahari ya Galilaya. Akapanda kilimami, akaketi huko. Wakamjia watu wengi sana, wakiwaleta wenye kupooza, viwete, vipofu, bubu, na wengine wengi. Wakawaweka miguuni pake. Naye akawaponya. Watu wakashangaa walipowaona bubu wanaongea, wenye kupooza wanapata afya, viwete wanatembea, na vipofu wanaona. Wakamtukuza Mungu wa Israeli. Yesu akawaita wafuasi wake, akasema, "Nauhurumia umati huu wa watu. Siku tatu wameshinda kwangu. Sasa hawana chakula. Sipendi kuwaaga wakiwa wanafunga, wasije wakazimia njiani." Wafuasi wake wakamwambia, "Hapa nyikani tupate wapi mikate mingi ya kuwashibisha watu wengi kama hawa?" Yesu akawauliza, "Mna mikate mingapi?" Wakamjibu, "Saba, na samaki wachache." Akawaamuru watu wakae chini. Akaitwaa ile mikate saba na wale samaki, akashukuru, akaimega akawapa wafuasi wake, nao wafuasi wakawapa watu. Wote wakala wakashiba. Wakakusanya makombo yaliyosalia, makapu saba yakajaa.
Injili ya Bwana.