SOMO 1
Isaya 63:16b-17, 19b; 64:2b-7
Wewe, Ee Bwana, ndiwe Baba yetu, mkombozi wetu, ndilo jina lako tangu milele! Ee Bwana, kwanini umetuacha sisi kutangatanga mbali na njia zako, mioyo yetu kuwa migumu hata hatukuabudu tena? Urudi, kwa ajili ya watumishi wako, na makabila yaliyo urithi wako. Kama ungepasua mbingu na kushuka chini, milima ingetetemeka mbele yako. Ulipotenda miujiza isiyotazamiwa, ulishuka nayo milima ilitetemeka mbele yako. Hakuna mtu aliyearifiwa wala kusikia, hakuna jicho lililoona Mungu yeyote ila wewe tu, alitenda hivyo, kwa ajili ya waamini wake. Wewe unawaendea kuwapokea watenda mema kwa furaha, wale wanaokujali wewe wanapofuata njia zako! Tulipokuwa tukitenda dhambi, ulikasirika juu ya watendao maovu, lakini tutaokoka. Sisi wote tulikuwa kama watu wachafu mbele yako, matendo yetu mema yalikuwa kama nguo chafu; wote tulikuwa tumekauka kama majani, makosa yetu yametupeperusha kama upepo. Hakuna hata mmoja aliyetaja jina lako, wala mtu aliyeamka ashikamane nawe; maana ulituficha uso wako mbele yetu, na kutuacha katika enzi ya maovu yetu. Lakini, ee BWANA, ndiwe Baba yetu; nasi ni udongo, wewe ndiwe mfinyanzi wetu: sisi sote tu kazi ya mikono yako.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 80:2ac na 3b, 15_16a, 18—19 (K. 4)
K. Ee Mungu, utuangazishie uso wako, nasi tutaokoka.
Ewe mchungaji wa Israeli, usikilize,,
uketiye juu ya makerubi ujionyeshe,
uamshe nguvu zako kuu, uje,
utusaidie tuwe salama. K.
K. Ee Mungu, utuangazishie uso wako, nasi tutaokoka.
Ee Mungu wa majeshi, urudi;
uangalie toka mbinguni, uone;
uje kuutazama mzabibu wako,
mche ulioupanda kwa mkono wako wa kulia. K.
K. Ee Mungu, utuangazishie uso wako, nasi tutaokoka.
Msaada wako na uwe juu ya mtu
aliye mkono wako wa kulia,
juu ya mwanadamu uliyemtia nguvu kwa ajili yako.
Basi hatutakuacha tena kamwe;
utatuhuisha tena, nasi tutaliitia jina lako. K.
K. Ee Mungu, utuangazishie uso wako, nasi tutaokoka
SOMO 2
1 Wakorintho 1:3—9
Ndugu zangu: Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo ziwe nanyi. Namshukuru Mungu wangu daima kwa ajili yenu, kwa sababu ya neema ya Mungu mliyopewa katika Kristo Yesu. Ndiyo maana katika yeye mmetajirika katika yote, katika kila neno na kila utambuzi. Kwa hiyo, ushuhuda wa Kristo umethibitika ndani yenu. Hivyo hamkosi kipaji cha Roho ninyi mnaotazamia kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Naye atawaimarisheni mpaka mwisho, msiwe na kosa siku ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni Mungu mwaminifu aliyewaita katika ushirika wa Mwanawe Yesu Kristo, Bwana wetu.
Neno la Bwana.
SHANGILIO LA INJILI
ZABURI 85:8
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Utuonyeshe wema wako, ee Bwana; utuletee wokovu wako.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 13:33—37
Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake: "Angalieni! Kesheni! Kwa maana hamjui wakati wa kutendeka hayo. Ni kama kwa mtu aliyetoka nyumbani aende safarini. Anawapa watumishi wake mamlaka, kila mmoja kazi yake, na bawabu amemwamuru akeshe. Kesheni basi, kwa maana hamjui bwana wa nyumba atarudi lini, labda jioni, au katikati ya usiku, au wakati wa kuwika jogoo, au alfajiri. Akifika ghafla, asiwakute mmelala usingizi. Ninayowaambia ninyi, nawaambia watu wote: 'Kesheni!'"
Injili ya Bwana