SOMO 1
Danieli 7:15—27
Mimi, Danieli, nilisongwa sana rohoni, na hayo maono yangu yalinihangaisha kabisa. Nikamkaribia mmoja wa wale waliosimama mbele ya Mungu, akanijulisha maelezo ya kweli ya hayo yote; akanijibu, akanijulisha maelezo ya mambo hayo: "Wale wanyama wanne wakubwa ni wafalme wanne watakaotokea duniani. Lakini watakatifu wa yule Aliye Juu watapokea ufalme na kuulinda milele na milele." Baadaye nikamwuliza maana hakika ya yule mnyama wa nne, aliyekuwa wa namna tofauti na wanyama wengine wote. Huyo alikuwa mwenye kutisha kabisa, mwenye meno ya chuma na miguu ya shaba nyekundu, naye alikula na kuponda, akakanyaga kwa miguu yake yale yaliyobaki; nikamwuliza na maana ya zile pembe kumi zilizokuwa kichwani mwake, na ya ile pembe iliyotokea, na mbele yake pembe tatu zikang'olewa; na kuhusu pembe nyingine zote. Nilikuwa nimeona ile pembe yenye kufanya vita na watakatifu na kuwatawala kwa nguvu, mpaka alipokuja yule Mzee wa Kale aliyewapatia hukumu watakatifu hao waliopewa ufalme. Naye akasema hivi, "Yule mnyama wa nne ni ufalme wa nne utakaotokea duniani. Ufalme huo utakuwa wa namna tofauti na falme nyingine zote; nao utakula dunia yote, na kuiponda na kuisaga kabisa. Pembe zile kumi ni wafalme kumi watakaotokea katika ufalme huo; mfalme mwingine atatokea baada ya hao, atakuwa wa namna tofauti na wale waliomtangulia, naye atawashusha wafalme watatu. Atasema maneno ya kiburi juu ya yule Aliye Juu, atawafanyia mabaya watakatifu wa yule Aliye Juu, atakusudia kubadilisha nyakati na sheria. Nao watakatifu watatolewa mikononi mwake, muda wa wakati na nyakati na nusu ya wakati. Lakini wenye kuhukumu barazani wakaketi, na mfalme huyo ataondolewa utawala wake, nao utaaibishwa na kuangamizwa hata milele, nalo taifa la watakatifu wa yule Aliye Juu litapewa ufalme na ukuu na utawala juu ya falme zote zilizoko chini ya mbingu. Ufalme wake ni ufalme wa milele, na falme zote zitamtumikia na kumtii."
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
DANIELI 3:60, 61, 62, 63, 64, 65 (K. 60b)
K. Msifuni na kumtukuza milele.
Enyi wana wa watu, mtukuzeni Bwana,
msifuni na kumtukuza milele. K.
Ewe nyumba ya Israeli, mtukuzeni Bwana,
msifuni na kumtukuza milele. K.
Enyi makuhani, mtukuzeni Bwana,
msifuni na kumtukuza milele. K.
Enyi watumishi wake, mtukuzeni Bwana,
msifuni na kumtukuza milele. K.
Enyi mioyo na roho za watu wema, mtukuzeni Bwana,
msifuni na kumtukuza milele. K.
Enyi roho na mioyo ya wenye haki, mtukuzeni Bwana,
msifuni na kumtukuza milele. K.
Enyi watakatifu na wanyenyekevu wa moyo, mtukuzeni Bwana,
msifuni na kumtukuza milele. K
SHANGILIO LA INJILI
LUKA 21:36
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Kesheni na kusali daima, mpate kusimama mbele ya Mwana wa Mtu.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 21:34—36
Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake, "Basi, jihadharini, mioyo yenu isije ikaelemewa na anasa, na ulevi, na shughuli za maisha, na siku ile ikawajia ghafla, maana kama tanzi itawapata wote wanaoishi duniani kote. Basi, kesheni na kusali daima, mpate nguvu ya kuepuka matukio hayo yote yatakayokuja, na kusimama mbele ya Mwana wa Mtu."
Injili ya Bwana.