Isaya 52:7—10
Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima miguu yake aletaye habari njema na kutangaza amani, aletaye habari ya heri na kutangaza wokovu, anayeuambia Sioni, "Mungu wako atawala!" Sikiliza walinzi wako wanapaza sauti, wanalia pamoja kwa furaha; maana wataona jicho kwa jicho jinsi Bwana anavyorudi Sioni. Shangilieni kwa furaha, enyi wakiwa wa Yerusalemu! Maana Bwana atawatuliza watu wa taifa lake, anaukomboa Yerusalemu. Bwana anaufunua mkono wake mtakatifu mbele ya macho ya mataifa yote; na miisho yote ya dunia itauona wokovu wa Mungu wetu.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 98:1, 2—3ab, 3cd—4, 5—6 (K. 3c)
K. Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
kwa maana amefanya mambo ya ajabu,
mkono wake wa kulia, na mkono wake mtakatifu,
umemletea ushindi. K.
Bwana ameujulisha ushindi wake;
mbele ya macho ya mataifa ameifunua haki yake,
amekumbuka wema na uaminifu wake
kwa nyumba ya Israeli. K.
Miisho yote ya dunia imeuona
wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote;
pigeni kelele za furaha; imbeni zaburi. K.
Mwimbieni Bwana kwa kinubi,
kwa kinubi na sauti ya vinanda.
Kwa tarumbeta na sauti ya baragumu
shangilieni mbele ya Mfalme, Bwana. K.
SOMO 2
Waebrania 1:1—6
Nyakati zilizopita, mara nyingi na kwa namna nyingi, Mungu alisema na mababu zetu kwa njia ya manabii. Siku hizi za mwisho amesema nasi kwa njia ya Mwanae, aliyemweka kuwa mrithi wa vyote, na kwa njia yake aliuumba ulimwengu. Huyu ni mng'ao wa utukufu wake na mfano wa hali yake, na ambaye anauhifadhi ulimwengu wote kwa neno la uwezo wake. Na baada ya kufuta dhambi, ameketi mkono wa kulia wa Mtukufu wa mbinguni. Ametukuka kupita malaika kwa kadiri ya jina alilolirithi linavyopita lao. Je, Mungu alimwambia malaika gani mmoja wapo: "Wewe u mwana wangu, mimi nimekuzaa leo?" Au: "Mimi nitakuwa kwake Baba, na yeye atakuwa kwangu mwana?" Tena baada ya kumwingiza mzaliwa wa kwanza hapa duniani, anasema: "Malaika wote wa Mungu wamwabudu."
SHANGILIO LA INJILI
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Siku takatifu imetung'aria:
enyi mataifa njoni mkamwabudu Bwana, kwa sababu leo mwanga mkubwa umeshuka duniani.
W. Aleluya.
INJILI
Yohane 1:1—18
Mwanzoni kulikuwako Neno, naye alikuwa kwa Mungu. Na Neno huyu alikuwa Mungu. Huyu mwanzoni alikuwako kwa Mungu. Kwa Neno vyote vimeumbwa, na pasipo Neno hakikuumbwa chochote kilichoumbwa. Ndani yake ulikuwamo uzima, na uzima ulikuwa ni mwanga wa wanadamu; na mwanga huo uliangaza gizani, lakini giza halikuupokea. Palitokea mtu, ametumwa na Mungu, jina lake Yohane. Huyu alikuja kutoa ushuhuda, apate kuushuhudia mwanga ili wote wasadiki kwa sababu yake. Yeye hakuwa ule mwanga, ila wajibu wake ulikuwa kuushuhudia ule mwanga. Alikuwako mwanga halisi amwangazaye kila mtu, alikuwa ulimwenguni humu. Alikuwako ulimwenguni, nao ulimwengu uliumbwa kwa njia yake, lakini ulimwengu haukumtambua. Alifika kwa walio wake, nao walio wake hawakumpokea. Lakini wote waliompokea aliwapa uwezo wa kuwaa watoto wa Mungu, ndio wale wasadikio kwa jina lake, waliozaliwa, si kwa damu, wala tamaa ya mwili, wala kwa tamaa ya mwanadamu bali kwa mapenzi ya Mungu. Neno akafanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tumeuona utukufu wake, utukufu kama wa mzaliwa wa pekee wa Baba, amejaa neema na kweli. * Yohane alimshuhudia na alipaza sauti yake akasema, "Huyu ndiye niliyemtaja niliposema, 'Anayekuja nyuma yangu amekuwa mbele yangu, kwa maana alikuwa kabla yangu.'" Katika ukamilifu wake sisi sote tumepokea neema juu ya neema. Kwa maana sheria imetolewa kwa njia ya Musa, lakini neema na kweli zimepatikana kwa Yesu Kristo. Hakuna aliyemwona Mungu. Mwana pekee, Mungu, aliye kifuani mwa Baba, amemtambulisha kwetu.
Injili ya Bwana.