MASOMO YA MISA, KUMBUKUMBU YA MT. INYASI WA LOYOLA, PADRE, JULAI 31, 2024
RANGI YA KILITURJIA: NYEUPE 🤍
SOMO LA KWANZA
YEREMIA 15:10, 16—21
Mbona mateso yangu hayana mwisho? Ukirudi na kunitumainia, utakaa imara mbele yangu.
Somo katika kitabu cha Nabii Yeremia
Ole wangu, mama yangu, kwa kuwa ulinizaa! Mimi ni mtu mwenye ugomvi na kushindana na nchi yote! Mimi sikukopesha wala sikukopa, hata hivyo wote wananiapiza. Palipopatikana maneno yako, niliyatafuna; neno lako lilikuwa furaha yangu na shangilio la moyo wangu, maana nimeitwa kwa jina lako, ee Bwana, Mungu wa majeshi. Sikuketi katika mkutano wa wale wanaofurahi, wala sikujiburudisha pamoja nao; niliketi peke yangu, nikishurutishwa na mkono wako, kwa maana umenijaza hasira kuu. Mbona mateso yangu hayana mwisho, na kidonda changu hakiponyeki, bali kinakataa kupona? Umekuwa kwangu kama kijito kidanganyifu, kama maji nisiyoweza kuyatumainia! Lakini Bwana amesema hivi: Ukirudi na kunitumainia, mimi nitakurudisha, utakaa imara mbele yangu; nawe ukisema maneno bora na kuyaacha maneno yasiyofaa, utakuwa kama kinywa changu mwenyewe, Wao. watakurudia wewe, bali si juu yako kuwarudia hao. Juu ya taifa hili nitakufanya wewe ukuta wa shaba nyekundu ulio wa nguvu. Wao watashindana nawe, lakini hawatakuweza hata kidogo. Maana mimi nitakuwa pamoja nawe, ili nikuokoe na kukukomboa, asema Bwana. Nitakuopoa katika mikono ya waovu, nitakukomboa katika mkono wenye jeuri.
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 59:2—3, 4—5a, 10—11, 17, 18
K. Mungu ndiye ngome yangu wakati wa shida.
Uniopoe na adui zangu, ee Mungu wangu;
unikinge na wenye kunishambulia.
Uniopoe na watu waovu,
uniokoe na watu wa damu. K.
Maana, tazama, wanaiotea nafsi yangu;
watu wakatili wanakula njama dhidi yangu,
si kwa kosa langu, wala si kwa dhambi yangu, ee Bwana!
Bila kosa langu, wanakuja mbio na kujiweka tayari. K.
Ee nguvu yangu, ninakutazamia.
maana Mungu, ndiwe ngome yangu, Mungu anipendaye.
Mungu wa fadhili zangu atanitangulia.
Mungu atanijalia kuona adui zangu wameangamia. K.
Nami nitauimba uweza wako,
na asubuhi nitazishangilia fadhili zako,
kwa maana umekuwa ngome yangu,
na kimbilio siku ya shida yangu. K.
Ewe nguvu yangu, nitakuimbia kwa shangwe,
maana Mungu, ndiwe ngome yangu,
Mungu wa fadhili yangu. K.
SHANGILIO LA INJILI
YOHANE 15:15b
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mimi nawaita rafiki, asema Bwana, kwa kuwa nimewajulisha yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu.
W. Aleluya.
SOMO LA INJILI
MATHAYO 13:44—46
Aliuza mali yake yote, akalinunua lile shamba.
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo
Wakati ule: Yesu aliwaambia makutano, "Ufalme wa mbingu umefanana na hazina iliyofichika shambani. Mtu alipoigundua, aliificha tena, kwa furaha juu yake akaenda, akauza mali yake yote, akalinunua lile shamba. Tena ufalme wa mbingu umefanana na mfanya biashara atafutaye lulu nzuri. Alipoiona moja ya thamani kubwa, alikwenda, akauza mali yake yote, akainunua."
INJILI YA BWANA... SIFA KWAKO EE KRISTO