MASOMO YA MISA, JUMAMOSI YA JUMA LA KUMI NA SITA, KIPINDI CHA KAWAIDA, MWAKA II, JULAI 27, 2024
RANGI YA KILITURJIA: KIJANI KIBICHI 💚
SOMO LA KWANZA
YEREMIA 7:1—11
Nyumba hii iitwayo kwa jina langu, je, imekuwa machoni penu pango la wanyang 'anyi?
Somo katika kitabu cha Nabii Yeremia
Neno la Bwana lilimfikia Yeremia likisema: "Simama langoni pa hekalu la Bwana na kutangaza pale neno hili: Sikilizeni neno la Bwana, enyi wote, watu wa Yuda wenye kuingia katika milango hii ili mwende kumwabudu Bwana. Bwana wa majeshi. Mungu wa Israeli amesema hivi: Shikeni njia safi zaidi, muwe na mwendo mwema zaidi, nami nitakaa nanyi mahali hapa. Wala msiyatumainie maneno ya uongo mkisema, Hekalu la Bwana! Hekalu la Bwana! Hekalu la Bwana! Lakini ikiwa mtashika njia safi zaidi, na kuwa na mwendo mwema zaidi: ikiwa mtatenda yaliyo haki kila mtu kwa jirani yake; ikiwa hamtamdhulumu mgeni wala yatima wala mjane; ikiwa hamtamwaga mahali hapa damu isiyo na kosa, ikiwa hamtafuata miungu mingine kwa upotevu wenu wenyewe, hapo nitawakalisha ninyi mahali hapa, katika nchi niliyowapa baba zenu tangu milele na hata milele. Lakini tazameni: mnayatumainia maneno ya uongo na ya bure, kwa maangamizi yenu! Je, mnaweza kuiba na kuua, kuzini na kuapa kwa uongo, kumfukizia ubani Baali, kuwafuata miungu wa kigeni msiowajua, na kisha mje hapa na kusimama mbele yangu katika nyumba hii inayoitwa kwa jina langu na kusema:Tuko salama! Tunaweza kufanya machukizo hayo yote tena? Nyumba hii iitwayo kwa jina langu, je, imekuwa machoni penu pango la wanyang'anyi? Tazameni, mimi mwenyewe nimeiona kuwa vile, asema Bwana.
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 84:3, 4, 5—6a, 1l (K. 2)
K. Maskani zako zapendeza kama nini, ee Bwana wa majeshi!
Nafsi yangu inazitamani nyua za Bwana hata inataka kuzimia.
Moyo wangu na mwili wangu vinamlilia Mungu aliye hai. K.
Kama ndege aliyepata nyumba,
na mbayuwayu kupata kiota cha kuwekea makinda yake,
maskani yangu yapo katika altare zako, ee Bwana wa majeshi,
Mfalme wangu na Mungu wangu! K.
Wana heri wale wanaokaa nyumbani mwako!
Wanakusifu daima.
Heri mtu anayepata nguvu kwako
anayetamani kupanda hekaluni mwako, K.
Kweli, siku moja katika nyua zako
ni bora kuliko nyingine elfu.
Afadhali zaidi kuwa bawabu nyumbani mwa Mungu wangu,
kuliko kukaa hemani mwa wenye dhambi. K.
SHANGILIO LA INJILI
YAKOBO 1:21bc
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Lipokeeni kwa upole neno lililopandwa ndani mwenu, ndilo neno liwezalo kuokoa roho zenu.
W. Aleluya.
SOMO LA INJILI
MATHAYO 13:24—30
Ziacheni mbegu zote mbili zikue pamoja mpaka wakati wa mavuno.
†Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo
Wakati ule: Yesu aliwasimulia watu mfano mwingine akisema, "Ufalme wa mbingu umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika shamba lake. Lakini watu walipolala usingizi, adui yake akaja, akapanda magugu kati ya ngano, akaenda zake. Miche ilipomea na kuchanua, magugu pia yakaonekana. Hapo watumishi wa mwenye shamba wakamwendea na kumwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika shamba lako? Limepataje magugu?' Akawaambia, 'Adui amefanya haya.' Watumishi wakamwuliza, Je, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La, sivyo, msije mkang'oa ngano pamoja na magugu mnayotaka kukusanya. Ziacheni mbegu zote mbili zikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Na wakati wa mavuno nitawaambia wavunaji, Kusanyeni kwanza magugu, mkayafunge matita matita na kuyachoma moto, Na kisha
hapo kusanyeni ngano ghalani mwangu.
INJILI YA BWANA... SIFA KWAKO EE KRISTO