MASOMO YA MISA, AGOSTI, 3, 2024
RANGI YA KILITURJIA: KIJANI KIBICHI 💚
SOMO LA KWANZA
YEREMIA 26:11—16, 24
Bwana amenituma kweli kwenu kuwaambia ninyi maneno hayo yote.
Somo katika kitabu cha Nabii Yeremia
Siku zile: Makuhani na manabii waliwaambia wakuu na watu wote, "Mtu huyu amestahili kufa! Ametoa unabii juu ya mji huu, kama mlivyosikia kwa masikio yenu wenyewe." Hapo Yeremia akasema na wakuu na watu wote, akawaambia, "Bwana ndiye aliyenituma kutoa unabii juu ya hekalu hili na mji huu, na kusema maneno yote mliyosikia. Sasa basi mgeuze njia zenu na matendo yenu; msikilize sauti ya Bwana, Mungu wenu, ili Bwana ajute na kuacha mabaya aliyoyanena juu yenu. Kwangu mimi, tazama, nipo hapa mikononi mwenu; mnifanyizie kama mnavyoona kuwa vyema na sawa machoni penu. Lakini mjue vema kwamba, mkiniua, mtajiletea damu isiyo na kosa juu yenu na juu ya mji huu na wakaaji wake. Kwa sababu Bwana amenituma kweli kwenu, kuwaambia ninyi maneno hayo yote. Hapo wakuu na watu wote wakawaambia makuhani na manabii. Mtu huyu hastahili kufa, kwa sababu amesema nasi kwa jina la Bwana, Mungu wetu." Yeremia mwenyewe alilindwa na Ahikamu mwana wa Shafani, asije akakamatwa na watu na kuuawa nao.
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 69:15—16, 30—31, 33—34
K. Ee Bwana, unijibu kwa wingi wa fadhili zako.
Uniopoe katika matope nisizame:
uniokoe katika wale wanaonichukia.
na katika vilindi vya maji.
Mawimbi ya maji yasinichukue.
wala kilindi kinimeze,
wala shimo lifunge kinywa chake juu yangu. K.
Nami, niliye mnyonge na mgonjwa,
Ee Mungu, wokovu wako unilinde.
Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo;
nitamtukuza kwa kumtolea shukrani. K.
Enyi maskini, tazameni, furahini,
enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe!
Maana Bwana huwasikia wahitaji.
wala hawadharau wafungwa wake. K.
SHANGILIO LA INJILI
MATHAYO 5:10
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Heri wenye kudhulumiwa kwa ajili ya haki kwa maana ufalme wa mbingu ni wao.
W. Aleluya.
SOMO LA INJILI
MATHAYO 14:1—12
Herodi alimtuma mtu gerezani amkate Yohane kichwa; wafuasi wake wakaenda kumpasha Yesu habari.
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo
Wakati ule: Herode Tetraki alisikia habari za Yesu. Akawaambia watumishi wake, "Huyo ndiye Yohane Mbatizaji. Amefufuka katika wafu. Kwa hiyo nguvu za kutenda miujiza zimo ndani yake." Kwa maana Herode alikuwa amemkamata Yohane, akamfunga na kumtia gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa ndugu yake, Filipo. Kwani Yohane alimwambia, "Si halali kwako kuwa naye. Alitaka kumwüa, lakini aliwaogopa watu, kwa sababu waliamini kuwa ni nabii. Baadaye walipoadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia alicheza mbele yao, akampendeza Herode sana, hata akaahidi kwa kiapo, kwamba atampa lolote atakaloliomba. Naye kwa ushauri wa mama yake, akasema, Nipe sasa hivi katika sahani kichwa cha Yohane Mbatizaji." Mfalme akasikitika. Lakini kwa sababu ya viapo vyake, na kwa ajili ya wageni wake karamuni, aliamuru apewe. Akamtuma mtu gerezani amkate kichwa Yohane. Kichwa chake kikaletwa katika sahani na akapewa msichana. Naye akakipeleka kwa mama yake. Wanafunzi wake wakaja kuichukua maiti na kuizika. Kisha wakaenda kumpasha Yesu habari.
INJILI YA BWANA... SIFA KWAKO EE KRISTO