MASOMO YA MISA, AGOSTI 2, 2024
RANGI YA KILITURJIA: KIJANI KIBICHI 💚
SOMO LA KWANZA
YEREMIA 26:1—9
Hapo watu wote wakamkusanyikia Yeremia katika nyumba ya Bwana.
Somo katika kitabu cha Nabii Yeremia
Mwanzo wa utawala wa Yehoiakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili lilifika kutoka kwa Bwana, likisema: “Bwana asema hivi: Nenda ukasimame katika uwanja wa nyumba ya Bwana, ukaseme juu ya miji yote ya Yuda inayokuja kuabudu katika hekalu la Bwana, ukaiambie maneno yote niliyokuagiza kuiambia, wala usiache hata neno moja. Labda watasikiliza, watarudi kila mtu akiacha njia yake mbaya, nami nitajuta na kuacha mabaya niliyokusudia kuwatendea, kwa sababu ya uovu wa matendo yao. Uwaambie: Bwana amesema hivi: Kama hamnisikilizi, wala hamwendi kwa kushika sheria yangu niliyoweka mbele yenu, kama hamsikilizi maneno ya manabii, ndio watumishi wangu ninaowatuma kwenu, ninaowatuma asubuhi na mapema, wala ninyi hamwasikilizi, basi mimi nitafanya hekalu hili kuwa kama Shilo, na mji huu nitaufanya
uapizwe na mataifa yote ya dunia." Makuhani, manabii na watu wote wakamsikia Yeremia anasema maneno hayo katika nyumba ya Bwana. Ikawa, Yeremia alipomaliza kusema maneno yote Bwana aliyomwagiza kuwaambia watu wote, makuhani na manabii na watu wote walimkamata, wakisema, Kufa, utakufa! Mbona umetoa unabii kwa jina la Bwana ukisema, "Nyumba hii itakuwa kama Shilo, na Mji huu utabomolewa, wala hautakaliwa tena na mtu'?" Hapo watu wote wakamkusanyikia Yeremia katika nyumba ya Bwana.
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 69:5, 8—10, 14 (K. 14c)
K. Kwa wingi wa rehema yako unijibu, ee Bwana.
Wenye kunichukia bila sababu ni wengi
kuliko nywele za kichwa changu.
Adui zangu wanaotaka kunimaliza
kwa mambo yasiyo kweli.
Nirudisheje vitu nisivyopokonya? K.
Maana kwa ajili yako ninavumilia fedheha,
aibu imenifunika uso wangu.
Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,
mtu asiyejulikana kwa wana wa mama yangu.
Maana wivu wa nyumba yako umenimaliza,
laumu zao wanaokutukana wewe zimenipata. K.
Sala yangu inakuelekea, ee Bwana,
wakati wa neema yako.
Ee Mungu, unisikilize kwa wema wako mkubwa,
kwa uaminifu wako wenye kuniokoa. K.
SHANGILIO LA INJILI
1 PETRO 1:25
K, Aleluya. W. Aleluya.
K Neno la Bwana ladumu milele, ndilo neno mlilohubiriwa katika habari njema.
W. Aleluya.
SOMO LA INJILI
MATHAYO 13:54—58
Je, huyu si mwana wa serenmala? Basi, hayo yote ameyapata wapi?
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo
Wakati ule: Yesu alienda nyumbani kwake. Huko aliwafundisha watu katika sinagogi lao, hata wakashangaa na kusema, "Amepataje hekima hii na uwezo wa miujiza? Je, huyu si mwana wa seremala? Na mama yake haitwi Maria? Na kaka zake si Yakobo, Yosefu, Simoni, na Yuda? Na dada zake wote hawakai nasi hapa petu? Basi, hayo yote ameyapata wapi?" Wakakwazika kwake. Yesu akawaambia, "Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika mji wake na nyumbani mwake." Huko hakufanya miujiza mingi kwa sababu ya ukosefu wao wa imani.
INJILI YA BWANA... SIFA KWAKO EE KRISTO