RANGI YA KILITURJIA: KIJANI KIBICHI 💚
SOMO LA KWANZA
NAHUMU 2:1, 3; 3:1—3, 6—7
Ole wake, mji wa damu.
Somo katika kitabu cha Nabii Nahumu
Tazama, juu ya milima, miguu ya yule aletaye habari njema, atangazaye amani! Ee Yuda, adhimisha sikukuu zako, zitimize nadhiri zako: kwa maana, yule mwovu hatapita tena kwako kamwe, amekatiliwa mbali kabisa. Hakika Bwana atairudisha tena fahari ya Yakobo, kama ile fahari ya Israeli; ingawa wateka nyara wamewateka, na kuharibu matawi ya mizabibu yao. Ole wake, mji wa damu, uliojaa uongo na unyang'anyi, usiokaa bila mateka. Sikia sauti ya mjeledi na sauti ya magurudumu yanayofanya kishindo, sauti ya farasi wenye kupiga shoti, sauti ya magari yenye kurukaruka. Mpanda farasi akwea kwa mori, na upanga ukimetameta, na mkuki uking'aa! Waliouawa ni wengi na mlundikano wa maiti, kuna mizoga isiyohesabika; wanajikwaa juu ya mizoga yao. Nitakutupia takataka, na kukuaibisha mbele ya watu, usiwe na sifa tena. Hapo kila mmoja atakayekuona atakimbia na kusema: "Ninawi umeangamia; nani atakayeuonea huruma?" Mtu atautafutia wapi wafariji?
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
KUM 32:35cd—36ab, 39abcd, 41
K. Mimi ndimi mwenye kutoa mauti na uzima.
Siku ya kukoma kwao imekaribia,
nayo yaliyowekwa tayari kwao yanakuja mbio.
Kwani Bwana atawafanyia haki kabila lake:
atawahurumia watumishi wake. K.
Fahamu sasa kwamba mimi ndie niliye,
na kwamba hapana mungu ila mimi tu;
ndie mwenye kuwapo, ndie mwenye kutoa mauti na uzima,
nikiisha kupiga, ndie mwenye kuponya. K.
Kama nikiisha noa upanga wangu ung aao,
na mkono wangu ukiisha shika hukumu,
nitawatoza kisasi adui zangu,
na nitawalipisha wenye kunichukia. K.
SHANGILIO LA INJILI
MATHAYO 5:10
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Heri wanaodhulumiwa kwa ajili ya haki, kwa maana ufalme wa mbingu ni wao.
W. Aleluya.
SOMO LA INJILI
MATHAYO 16:24—28
Mtu atoe nini aifidie nafsi yake?
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo
Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake, "Mtu akitaka kuwa mfuasi wangu, ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa maana mtu akitaka kusalimisha nafsi yake, ataipoteza. Lakini mtu apotezaye nafsi yake kwa ajili yangu, ataipata. Kwani yamfaa mtu nini akipata dunia yote na kupoteza nafsi yake? Au mtu atoe nini aifidie nafsi yake? Kwa maana Mwana wa Mtu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika wake. Hapo atamlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Amin, nawaambieni, baadhi ya hawa wanaosimama hapa hawataonja mauti kabla ya kumwona Mwana wa Mtu akija katika ufalme wake."
INJILI YA BWANA... SIFA KWAKO EE KRISTO