SOMO 1
Isaya 40:1—5, 9—11
Watulizeni, wapeni tulizo watu wangu, asema Bwana wenu. Semeni na moyo wa Yerusalemu, utangazieni ya kwamba: Huduma yake ngumu imekwisha, dhambi yake imeondolewa, maana kwa mkono wa Bwana amepokea adhabu maradufu kwa maovu yake yote. Mtu analia: tengenezeni jangwani njia ya Bwana! Nyosheni nyikani barabara kwa Mungu wetu! Kila bonde lifukiwe, kila na kilima kishushwe, njia zenye kupotoka zinyoshwe, na njia zenye mashimo zisawazishwe. Hapo utukufu wa Bwana utafunuliwa, na watu wote watauona mara; maana kinywa cha Bwana kimenena haya. Panda juu ya mlima mrefu, uitangaziye Sioni habari njema! Paza sauti kwa nguvu, uitangaziye Yerusalemu habari njema! Paza sauti, usiogope! Sema kwa miji ya Yuda: Tazama, Mungu wenu! Yupo hapa Bwana Mungu: anakuja kwa uwezo, na mkono wake utatawala; tuzo ya ushindi wake litamsindikiza, mateka yake yatamtangulia. Kama mchungaji, anachunga kundi lake; mkononi mwake atawakusanya wanakondoo, atawachukua kifuani mwake, atawaongoza kondoo wenye kunyonyesha.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 85:9ab—10, 11—12, 13—14 (K.
K. Utuonyeshe wema wako, ee Bwana; utupe wokovu wako.
Ninasikia anayosema Bwana Mungu;
hakika, anasema maneno ya amani
na watu wake na waamini wake.
Wokovu wake ni karibu nao wenye kumcha;
utukufu wake utakaa katika nchi yetu. K.
Wema na uaminifu zitakutana;
haki na amani zitabusiana.
Uaminifu utachipuka katika nchi;
na haki itachungulia kutoka mbinguni. K.
Naye Bwana atatoa yaliyo mema;
na nchi yetu itatoa mazao.
Haki itatangulia mbele ya Bwana,
wokovu utafuata nyayo zake. K.
SOMO 2
2 Petro 3:8—14
Ndugu wapendwa, msipitiwe katika jambo hili: siku moja kwa Bwana ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. Bwana hacheleweshi ahadi kama baadhi ya watu wanavyodhani 'anachelewa,' bali anawasubiria ninyi kwa sababu hapendi wengine wenu wapotee, bali wote watubu. Siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Hapo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikubwa; vitu vitaungua na kuteketea; dunia pamoja na matengenezo yake haitaonekana tena. Basi, vitu hivyo vikiharibiwa kwa namna hiyo, je haiwapasi ninyi kuishi kitakatifu zaidi na kumcha Mungu, kungoja na kuukimbilia ujio wa siku ya Mungu, ambapo mbingu zitakapoteketea moto na kutoweka, na viumbe vitakapoyeyushwa na kuteketezwa? Kisha tunatazamia — kama alivyoahidi — mbingu mpya na nchi mpya zenye uadilifu. Mkisubiri hayo, ndugu wapendwa, mjibidishe kuishi bila mawaa ili mkutwe katika amani.
Neno la Bwana.
SHANGILIO LA INJILI
LUKA 3:4, 6
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake, na kila kiumbe kitauona wokovu wa Mungu.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 1:1—8
Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya: "Tazama, namtuma mjumbe wangu; akutangulie na kukutayarishia njia. Ndiyo sauti ya mtu aliaye nyikani: 'Itayarisheni njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake.'" Yohane Mbatizaji alitokea nyikani akibatiza na kuutangaza ubatizo wa toba kwa maondoleo ya dhambi. Watu wa kutoka sehemu yote ya Yudea na wenyeji wote wa Yerusalemu, walikuwa wakimwendea kuungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani. Yohane alikuwa akivaa singa za ngamia, na mshipi wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. Alihubiri akisema, "Anayekuja baada yangu ni mwenye nguvu kunipita mimi. Kwake sifai hata kuinama na kumfungulia gidamu ya viatu vyake. Mimi nimewabatiza kwa maji; yeye lakini atawabatiza kwa Roho Mtakatifu."
Injili ya Bwana.