RANGI YA KILITURJIA: KIJANI KIBICHI 💚
SOMO LA KWANZA
1 WAFALME 19:4—8
Kutokana na nguvu ya chakula hicho, alisafiri hata akafika mlima wa Mungu.
Somo katika kitabu cha kwanza cha Wafalme
Siku zile: Eliya alienda siku nzima jangwani, hadi alipofika chini ya mti wa mzeituni, akaketi chini yake. Akasali akiomba kifo, "Sasa yatosha, ee Bwana! Uondoe uhai wangu, kwa maana mimi si mwema kuliko baba zangu." Akajilaza chini ya mretemu, akalala usingizi, lakini mara malaika akamgusa, akamwambia, "Simama, ule!" Akatazama, kumbe, akaona mkate umeokwa juu ya makaa, na gudulia la maji kichwani pake. Akala, akanywa na akajinyosha tena, malaika wa Bwana akaja mara ya pili, akamgusa, akasema, Simama, ule maana safari hii ni kubwa mno kwako!" Akasimama, akala, akanywa; na kutokana na nguvu ya chakula hicho, akasafiri kwa muda wa siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu mlima wa Mungu.
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 34:2—3, 4—5, 6—7, 8—9 (K. 9a)
K. Onjeni, mwone jinsi Bwana alivyo mwema.
Nitamtukuza Bwana kila wakati;
sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Nafsi yangu itajisifu katika Bwana
wanyonge wasikie na kufurahi. K.
Mtukuzeni Bwana pamoja nami:
tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nilimkimbilia Bwana, akanisikiliza,
akaniopoa katika hofu zangu zote. K.
Mtazameni Mungu mkafurahiwe
na nyuso zenu zisihuzunike.
Mnyonge huyu alilia, naye Bwana akamsikiliza,
akamwokoa katika shida zake zote. K.
Malaika wa Bwana ameweka kambi kwao,
kuwazungukia wale wamchao Mungu na kuwaokoa.
Onjeni, mwone jinsi Bwana alivyo mwema;
heri mtu yule anayemkimbilia. K.
SOMO LA PILI
WAEFESO 4:30—5:2
Mpendane daima kama Kristo alivyotupenda.
Somo katika barua ya Mtakatifu Paulo kwa Waefeso
Ndugu zangu: Msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu aliyewatia muhuri wake, mpate kuwa tayari siku ya ukombozi. Kila uchungu, hasira, chuki, kelele, matukano na kila aina ya ubaya viondoshwe kati yenu. Muwe wema ninyi kwa ninyi, mhurumiane na kusameheana kama Mungu alivyowasamehe ninyi katika Kristo. Hivyo fanyeni bidii kumwiga Mungu kama watoto wapenzi. Mpendane daima kama Kristo alivyotupenda na kujitoa sadaka kwa Mungu kwa ajili yetu, ndiyo harufu nzuri ya kumpendeza Mungu.
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
SHANGILIO LA INJILI
YOHANE 6:51
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mimi ndimi mkate wa uzima ulioshuka toka mbinguni, asema Bwana; aulaye mkate huu ataishi milele.
W. Aleluya.
SOMO LA INJILI
YOHANE 6:41—51
Mimi ndimi mkate wa uzima ulioshuka toka mbinguni.
†Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Yohane
Wakati ule: Wayahudi walimnung'unikia Yesu kwa sababu alisema, "Mimi ni mkate ulioshuka toka mbinguni." Wakasema, "Je, huyu si Yesu, mwana wa Yosefu? Twamjua baba yake na mama yake. Awezaje kusema Nimeshuka toka mbinguni?" Yesu akajibu, akawaambia, "Msinung'unike ninyi kwa ninyi. Hakuna awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho. Imeandikwa katika vitabu vya manabii: Wote watafundishwa na Mungu.' Kila amsikiaye Baba na kujifunza kwake anakuja kwangu. Si kwamba mtu amemwona Baba, ila yeye atokaye kwa Mungu; huyu ndiye aliyemwona Baba. Amin, amin, nawaambieni, anisadikiye anao uzima wa milele. Mimi ndimi mkate wa uzima. Baba zenu walikula mana jangwani, lakini wakafa; huu ndio mkate utokao mbinguni, ili mtu aulaye asife. Mimi ndimi mkate wa uzima ulioshuka toka mbinguni; aulaye mkate huu ataishi milele, na mkate nitakaotoa mimi ni mwili wangu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu."
INJILI YA BWANA... SIFA KWAKO EE KRISTO