MASOMO YA MISA, AGOSTI 4, 2024
RANGI YA KILITURJIA: KIJANI KIBICHI 💚
SOMO LA KWANZA
KUTOKA 16:2—4, 12—15
Nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni.
Somo katika kitabu cha Kutoka
Siku zile: Mkutano wote wa wana wa Israeli waliwanung'unikia Musa na Haruni huko jangwani. Wana wa Israeli wakawaambia, "Afadhali tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri, tulipoketi kwenye sufuria za nyama, tukala mkate tukashiba! Ninyi mmetuleta katika jangwa hili mpate kuua kwa njaa mkutano huu wote!" Bwana akamwambia Musa: Nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni. Watu watatoka wakusanye siku kwa siku sehemu ya kila siku. Nitawajaribu hivi, nipate kuona kama watafuata sheria zangu ama sivyo. Nimeyasikia manung'uniko ya wana wa Israeli. Basi waambie: Wakati wa jioni mtakula nyama, na asubuhi mtashiba mkate. Ndipo mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu." Kwa kweli, jioni ile, wakafika kware wakakifunika kituo, na kesho yake asubuhi umande ukatanda pande zote za kituo. Umande huo ulipotoweka pakaonekana juu ya jangwa kitu kama chembe chembe ndogo, chepesi na cheupe kama unga wenye kufunikia nchi. Kukiona, wana wa Israeli wakaambiana, "Nini hii?" Kwa maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, "Huo ndio mkate mliopewa na Bwana, uwe chakula chenu."
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 78:3 na 4bc, 23—24, 25 na 54 (K. 24b)
K. Bwana aliwapa mkate wa mbinguni.
Mambo tuliyosikia na kuyajua;
mambo ambayo baba zetu walituhadithia,
tutawaanmbia kizazi kijacho,
sifa za Bwana na nguvu yake. K.
Aliyaamuru mawingu ya anga;
akafungua milango ya mbingu.
Akawanyeshea mana awalishe;
akawapa ngano ya mbinguni. K.
Mwanadamu akala mkate wa malaika;
akawapa chakula tele.
Aliwafikisha katika nchi yake takatifu,
mpaka mlima aliotwaa kwa mkono wake wa kulia. K.
SOMO LA PILI
WAEFESO 4:17, 20—24
Mkavae utu mpya ulioumbwa kwa mfano wa Mungu.
Somo katika barua ya Mtakatifu Paulo kwa Waefeso
Ndugu zangu: Ninasema hili na kushuhudia katika Bwana kwamba hamuenendi tena kama watu wengine wa mataifa wanavyoenenda katika ubatili wa nia zao. Lakini mambo hayo hamkujifunza kwa Kristo, ikiwa mlimsikiliza na kuelimishwa ndani yake, jinsi neno la kweli lilivyo katika Yesu, imewabidi kuacha mwenendo wenu wa kwanza na kuvua utu wa zamani wenye kuharibika kwa kufuata tamaa potovu. Imewapasa kuwa watu wapya katika roho na maoni yenu. Mkamvae utu mpya ulioumbwa kwa mfano wa Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
SHANGILIO LA INJILI
MATHAYO 4:4b
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo kinywani mwa Mungu.
W. Aleluya.
SOMO LA INJILI
YOHANE 6:24—35
Ajaye kwangu hataona tena njaa, anisadikiye hataona tena kiu.
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Yohane
Wakati ule: Watu walipoona ya kuwa Yesu hayupo, wala wafuasi wake, waliingia vyomboni, wakaenda Kapernaumu wamtafute Yesu. Walipomwona ng'ambo ya bahari, walimwambia, "Rabbi, lini umefika hapa?" Yesu akawajibu, akawaambia, "Amin, amin, Waambieni, mnanitafuta, si kwa sababu mliziona ishara, ila kwa sababu mlikula mikate, mkashiba. Fanyeni bidii, si kwa kujipatia chakula kinachoharibika, bali kwa kujipatia chakula kinachodumu hata uzima wa milele. Chakula hicho atawapa Mwana wa Mtu; kwa maana huyo amekubaliwa na Baba, ndiye Mungu." Hapo wakamwambia, "Tufanyeje, ili tutende kazi za Mungu?" Yesu akajibu, akawaambia, "Hii ndiyo kazi ya Mungu, kumsadiki yule aliyetumwa na yeye." Wakamwambia, "Basi, utafanya ishara gani, tupate kuona na kusadiki? Utafanya nini? Baba zetu walikula mana jangwani, kama ilivyoandikwa: 'Aliwalisha mkate wa mbinguni.""Yesu akawaambia, “Amin, amin, nawaambieni, si Musa aliyewapa mkate toka mbinguni, bali ni Baba yangu awapaye mkate halisi toka mbinguni. Kwa maana mkate wa Mungu ni ule ushukao toka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima." Wakamwambia, "Bwana, utupe mkate huo siku zote." Yesu akawaambia, "Mimi ni mkate wa uzima; ajaye kwangu hataona tena njaa, anisadikiye hataona tena kiu."
INJILI YA BWANA... SIFA KWAKO EE KRISTO